NYUMBA za mfanyabiashara Saidi Lugumi zilizotangazwa kupigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart huenda zisiuzwe kwa sababu mfanyabiashara huyo naye anadaiwa kuidai serikali,

NYUMBA za mfanyabiashara Saidi Lugumi zilizotangazwa kupigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart huenda zisiuzwe kwa sababu mfanyabiashara huyo naye anadaiwa kuidai serikali, Raia Mwema limeambiwa.

Hivi karibuni, Yono ilitangaza kuuza nyumba tatu za Lugumi zilizopo jijini Dar es Salaam kwa maelezo kwamba anadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 14 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo ameshindwa kuzilipa katika muda uliokubaliwa.

Mnada wa kuuza nyumba hizo za kifahari zilizopo katika maeneo ya watu wenye ukwasi mkubwa umepangwa kufanyika Jumamosi Septemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili vimeeleza kwamba mnada huo unaweza kukwama kutokana na ukweli kwamba Lugumi mwenyewe anaidai serikali kiasi kikubwa cha fedha kuliko kile anachodaiwa na TRA.

“ Nafikiri mnada utasitishwa kwa sababu Lugumi naye anaidai serikali mabilioni ya shilingi kutokana na biashara alizowahi kufanya nayo katika miaka ya nyuma na bado hajalipwa hadi leo.

“ Sasa kiungwana mimi nakudai wewe shilingi kumi, kwa mfano. Wewe kama unanidai mimi shilingi tatu huwezi kuuza mali zangu kwa sababu mimi nakudai zaidi. Hiyo ndiyo hoja ambayo Lugumi anayo.

“ Mali zake zinataka kuuzwa na serikali ambayo anaidai kiasi kikubwa zaidi. Najua kwamba amewaambia badala ya kuuza mali zake, si wamlipe kwanza fedha anazoidai halafu yeye awalipe?,” mmoja wa marafiki wa Lugumi wanaofahamu vema biashara zake na serikali ameliambia gazeti hili.

Hadi tunakwenda mitamboni, haikuweza kufahamika ni biashara gani ambayo Lugumi alifanya na serikali yenye thamani hiyo ya mabilioni lakini Raia Mwema linafahamu kwamba mfanyabiashara alikuwa ni mmoja wa waliokuwa wakiaminiwa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa utawala wake.

Gazeti hili lilifanya jitihada zote za kuwasiliana na kumpata Lugumi hadi wakati tunakwenda mitamboni lakini juhudi zetu zote ziligonga mwamba. Tangu aanze kufahamika kutokana na biashara zake alizozifanya na Jeshi la Polisi kuanza kuchunguzwa na Bunge la Tanzania, Lugumi amekuwa mgumu kupatikana.

Gazeti hili lilizungumza na mmoja wa wasaidizi wake juzi lakini akaeleza kwamba bosi wake yuko katika vikao vya kikazi na atawasiliana na gazeti hili wakati atakapokuwa amemaliza. Hata hivyo, msaidizi huyo hakutaka kusema vikao hivyo vinafanyikia wapi na kama mwandishi wetu angeweza kwenda kumsubiri hukohuko.

Nyumba za Lugumi zinazotajwa ya kuwa zitapigwa mnada ni mbili zilizopo katika kiwanja namba 47 kitalu namba mbili Mbweni JKT Manispaa ya Kinondoni, kiwanja namba 57 kitalu namba mbili, kilichopo Mbweni na kiwanja namba 701/48 kilichopo Mtaa wa Mazengo, Upanga.

Akizungumza na Raia Mwema mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scolastica Kevela, alilieleza gazeti hili kwamba mpango wa kuzipiga mnada nyumba hizo uko palepale na hakuna taarifa zozote za kuzuia jambo hilo walizokuwa wamepata mpaka wakati huo.

“ Hadi ninavyozungumza na wewe muda huu sina taarifa yoyote kutoka TRA kueleza kwamba tusiuze hizi nyumba. Hivyo mnada wa Septemba 9 uko palepale labda kama mwenyewe atalipa deni lake kabla ya siku hiyo,” alisema Kevela mwishoni mwa wiki iliyopita.

Picha mbalimbali za televisheni zilizoonyeshwa wiki iliyopita katika vituo mbalimbali hapa nchini na kwenye mitandao ya kijamii zilimwonyesha mama huyo akiwa na kundi la wana habari kwenye baadhi ya nyumba zilizoelezwa kumilikiwa na Lugumi.

Kwa mujibu wa taratibu za madalali, endapo nyumba itauzwa, wanunuzi watatakiwa kulipa sehemu ya bei iliyokubalika kuuza nyumba hizo wakati wa mnada na kiasi kingine wakimalizie katika muda utakaokuwa umepangwa.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kwa sasa bado hawajajua majumba hayo ya kifahari watayauza kwa kiasi gani kwani wanasubiri kupewa bei elekezi na TRA ambao ndiyo wateja wao.

Akizungumzia jambo hilo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema suala la mnada wa nyumba hizo wameliacha kwa dalali ambaye ni Yono na kwamba taarifa zote kuhusu mnada huo zitatolewa na Yono wenyewe.

“ Suala la kusitishwa au kuendelea kwa mnada ni la dalali. Siwezi kuzungumzia jambo hilo kwa sasa kwa sababu tumemwachia mtu mwingine alishughulikie,” alisema Kayombo.

Kayombo hakutaka kusema kwa ujumla ni kiasi gani ambacho TRA inamdai Lugumi akisema kwamba suala hilo ni siri kati yao na mteja wao huyo na hakutaka pia kuzungumzia madai kwamba Lugumi naye anaidai serikali.

Lugumi ni nani?

Jina la Said Hamad Lugumi lilipata umaarufu wa ziada baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha ambazo kampuni yake ililipwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) katika vituo vya Polisi nchini.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilikuwa imeonyesha kwamba ingawa kampuni hiyo ilikuwa imepewa kandarasi ya ujenzi huo tangu mwaka 2011, ilikuwa haijakamilisha kazi hiyo ingawa ilikuwa imelipwa zaidi ya asilimia 90 ya gharama za kazi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka 2014/2015, kampuni ya Lugumi, Lugumi Enterprises ilikuwa imelipwa kiasi cha shilingi bilioni 34 kati ya shilingi bilioni 37 alizotakiwa kulipwa.

Si taarifa nyingi zinafahamika kumhusu Lugumi, ingawa anajulikana kuwa ni kijana aliyezaliwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na ametokea mbali kabla ya kuja kuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa.

LUGUMI na PAC

Kampuni ya Lugumi ilidaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Lakini hadi wakati PAC inaamua kulibeba suala hilo, mashine hizo zilikuwa zimefungwa katika vituo 14 pekee na kampuni hiyo kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za makubaliano ya mkataba.

Kutokana na hali hiyo, PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya ufisadi katika tenda hiyo, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili wajumbe waweze kuupitia pamoja na kutoa maagizo.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillary aliwaambia waandishi wa habari wakati sakata hilo la Lugumi likiwa limeshika kasi kwamba kamati yake iliwataka watendaji wa polisi kuwasilisha mkataba wa kampuni hiyo ili wajumbe waweze kuupitia na kutoa maagizo.

Alidai kwamba watendaji wa Jeshi la Polisi waliwasilisha taarifa ya mali tu, bila ya mkataba huo jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya kamati na kwamba suala la kuwaonyesha mkataba huo lilikuwa linapigwa danadana.

Alisema kamati hiyo inawasiliana na Katibu wa Bunge, Dk.Thomas Kashilila ili waweze kupata taarifa kama mkataba huo umewasilishwa ofisini kwake au laa.

Mbunge huyo wa Sumbawanga Mjini alisema kanuni za Bunge zinawataka watendaji wanaopewa maagizo ya kuwasilisha taarifa kwenye kamati, kuwasilisha taarifa hizo ofisi za Katibu wa Bunge.

“Kanuni za Bunge zinawataka watendaji kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwenye kamati kwa Katibu wa Bunge, ambaye akizipata anawasiliana na katibu wa kamati husika, lakini ninavyoongea na nyinyi hapa, hatujapewa taarifa yoyote kuhusu Lugumi,” alisema.

“Kama jeshi hilo halitawasilisha taarifa hiyo, kamati itaiagiza Serikali kuwachukulia hatua watendaji walioshindwa kutimiza wajibu wao.

“Hakuna cha kufichaficha hapa, ndiyo maana wajumbe wametaka mkataba huu kuwasilishwa, ikiwa Jeshi la Polisi litakaidi, tutaiandikia barua Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji waliokaidi agizo,” alisema Aeshi.

Alisema kutokana na hali hiyo, wajumbe wa kamati hiyo watasubiri taarifa hizo hadi ziweze kuwasilishwa, na ikiwa hazitawasilishwa watatoa tamko. Hatimaye PAC ilifanikiwa kuona mkataba huo.



Chanzo: Raia Mwema

Maoni