IGP SIRRO BADO ANATESEKA NA LISSU,AAMUA KUFUNGUKA,SOMA HAPO KUJUA


MKUU WA JESHI LA POLISI, IGP SIMON SIRRO

MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, amewataka wanasiasa wote nchini kuzingatia sheria na kwamba wasipofanya hivyo wataendelea kukamatwa kila uchao bila kujali majina wala nafasi zao.

IGP alisema miongoni mwa makosa yanayofanywa kila mara na wanasiasa ni pamoja na kuvunja sheria za nchi kwa kufanya mikutano isiyoruhusiwa.

Aidha, IGP Sirro alikanusha kuwa jeshi hilo limekuwa likiwakamata viongozi wa vyama vya upinzani wanapotekeleza majukumu yao  na kuwaacha wa chama tawala -- Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kufanya siasa nchini.

IGP Sirro aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari katika kikao chake kilichofanyika jana katika ofisi za TPC jijini Tanga, chanzo kikiwa ni madai ya upinzani yatokanayo na taarifa za kukamatwa kwao kila mara katika siku za hivi karibuni, akiwamo Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Wengine waliowahi kukamatwa na polisi hivi karibuni ni pamoja na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Akifafanua, IGP Sirro alisema jeshi lao litawakamata watu wote watakaovunja sheria za nchi huku akisisitiza kuwa jina la chama haliwezi kuwa sababu ya kukamatwa kwa mwanasiasa bali kitendo alichokifanya.

 “Aaah..! Wee bwana nani kakwambia wapinzani wanakamatwa wakifanya vikao vyao? Sisi tunaowakamata ni wanaovunja sheria na kwenye hilo huwa hatuangalii ni wa chama gani.

“Awe CCM tunakamata, awe Chadema, TLP tunakamata… kama kakosa tutamshughulikia,” alisema Sirro.

Katika kikao hicho, Sirro alielezea lengo la ziara yake mkoani Tanga kuwa ni pamoja na kuangalia utendaji wa jeshi hilo na changamoto zake pamoja na kuwakumbusha askari juu ya wajibu wao wa kusimamia sheria na kutenda haki.

Maoni