Kimbunga Harvey chazidi kusababisha maafa Texas, Marekani

Maafisa wa uokozi wanajaribu kuwaokoa watu kutoka manyumbani mwao na kwenye magari katika jimbo la Texas nchini Marekani baada ya kimbunga kilichopewa jina Harvey kuikumba miji kadhaa ya jimbo hilo kuanzia Ijumaa na kusababisha mafuriko makubwa. Maafisa hao wa uokozi wamewaokoa zaidi ya watu 1,000 katika eneo la Houston huku kimbunga hicho kikubwa zaidi kukumba Texas kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita kikizidi kusababisha maafa.Takriban watu wawili wameuawa na idadi ya walioathirika inatarajiwa kuongezeka kutokana na kimbunga hicho kuendelea kuwa na nguvu katika jimbo hilo. Maafisa wamewaonya wakazi dhidi ya kutoka majumbani mwao kwasababu barabara hazipitiki. Maelfu ya maafisa wa ulinzi wanasaidia katika shughuli za uokozi. Gavana wa Texas Greg Abbott ameonya hali inazidi kuwa mbaya jimboni humo.

Maoni