POLISI AMBAO WANASEMA TUMEPOKEA KAULI KUTOKA JUU AWAJIAMINI KATIKA UTENDAJI KAZI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema atahakikisha anakataa Dar es Salaam kuwa maficho ya watu wanaofanya uhalifu maeneo ya pembezoni na kukimbilia jijini humo na kubaki salama, pamoja na kuhakikisha jiji hilo siyo sehemu ya kuzalisha uhalifu.

Aidha, amewaomba wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na waandishi wa habari, kumpatia ushirikiano wa kutosha ili kukabiliana na uhalifu na kuifanya jamii kuishi katika hali ya amani na usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa kamanda wa kanda hiyo, Mambosasa alisema usalama wa jiji hilo unawezekana, endapo wananchi watatoa ushirikiano na kuacha kufumbia macho wahalifu, badala yake kuripoti matukio ya uhalifu kwa wakati.

Alisema hawezi kukubali Dar es Salaam ikawa ni sehemu ya watu kukimbilia baada ya kufanya uhalifu au kufanya uhalifu na kukimbilia maeneo ya pembezoni. 

“Ninataka Dar es Salaam iwe mahali salama pa kuishi na najua hayo hayawezi kufanyika bila ushirikiano wa wananchi ndo maana ninawaomba tupeane ushirikiano…taarifa za uhalifu kwangu ni mtaji wa kuzifanyia kazi,” alisema Kamanda Mambosasa ambaye wiki iliyopita aliteuliwa kushika wadhifa huo akitokea mkoani Dodoma kwa wadhifa huo.

Aliongeza, “Ninawaombeni ushirikiano na pote nilipopita nimekuwa na waandishi wa habari… Mimi nipo kwa ajili ya kupambana na uhalifu na naomba nisipimwe kwa vigezo vya ‘rank’ yangu kwamba nafasi niliyochukua ni ya watu wakubwa sana… hao ndiyo wamenipa hiyo kwa kuona ninatosha, nitatoa ushirikiano wa dhati na ninachoomba kwenu na kwa wananchi kwa ujumla ni suala la ushirikiano na kutoa taarifa za awali za uhalifu.”

Alisema atahakikisha anawatumia maofisa wanaofanya kazi na Jeshi la Polisi kwa kuweka mazingira rafiki na salama na wananchi ili kuondoa kero zinazowakabili na kuwafanya kushindwa kufanya shughuli za kuwaletea maendeleo.

“Nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote ili kuhakikisha kero za wananchi zinamalizwa na hili siyo suala la miujiza, bali ni suala la ushirikishwaji wa umma,” alisema Mambosasa. 

Alieleza, “mikakati yangu ni kwamba nina thamani ulinzi wa pamoja wa vyombo vya ulinzi na usalama, ninatambua kamati za ulinzi na usalama kuanzia kata hadi mikoa na viongozi wote wa vyama na serikali na viongozi wa makampuni binafsi ambao ni sehemu ya ulinzi na usalama… nitahakikisha nashirikisha watanzania wote kushiriki katika kuukataa uhalifu.”

Kamanda Mambosasa pia aliwaomba wananchi kutoa taarifa za uhalifu katika maeneo yao ili zifanyiwe kazi kwa wakati ili kutokomeza vitendo vya uhalifu, vinavyojitokeza kwa kutumia namba za simu 0756616777 na 0751009983.

Kamanda Mambosasa amewahi kufanya kazi Makao Makuu ya Polisi Kitengo cha Polisi Jamii, na katika mikoa ya Simiyu na Tarime/Rorya kwa nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa na aliwahi kuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Kimara, Hanang na Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala.

Maoni