HABARI MPYA KUTOKA KENYA MDA KUHUSU MH LISSU.

Muda huu, watu ambao wanaelezwa ni makachero wamewekwa katika Hospitali ya Agha Khan jijini Nairobi kuimarisha zaidi Ulinzi katika Hospitali hiyo aliyolazwa mbunge wa Singida Mashariki nchini Tanzania Tundu Lissu.
Mwandishi wa Habari wa kujitegemea Boinet Omuru aliyepo nchini Kenya, ameiambia kuwa eneo hilo linadhibitiwa vikali.
Hapa kuna ulinzi mkali, nimefika hapa kwa ajili ya habari kama mwandishi lakini mlolongo umekuwa mgumu, nimeshindwa kuzungumza sources za hapa”
Boinet anasema hakuna ubize wowote na wala hakuna watu wanaoingia hapo kwa urahisi katika eneo ambalo Tundu Lissu amelazwa.
Kuna utulivu mkubwa”
Yupo mke wake na ndiye mara nyingi anatoa ruhusa nani amsalimie mgonjwa.
Makachero wa hapa Kenya, wapo hapa wamevalia kiraia. Ukifika katika lango la kuingilia unaulizwa maswali mengi sana, ukitaka kupiga picha unazuiwa”
Viongozi wa vyama vya Mawakili kutoka Kenya, Uganda, Rwanda jana walifika Hospitalini hapo kumuona kiongozi huyo.
Makamu wa rais wa chama cha Mawakili Afrika, ambaye aliwahi kuwa rais wa chama cha Mawakili nchini Kenya,Eric Mutua, jana aliiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha inamuwekea Ulinzi kiongozi huyo ili watu waliojaribu kumuua wasimdhuru akiwa nchini humo.
”Hatuna uhakika kama waliojaribu kumuua nchini Tanzania hawatatekeleza mpango wao nchini Kenya. Ni muhimu bwana Lissu alindwe na maafisa wa Polisi wa Kenya” alisema Mutua
Hata hivyo Serikali ya Kenya haijazungumza hadharani, lolote juu ya maombi hayo.
Msemaji wa rais Uhuru Kenyatta Manoah Esipisu, alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia suala hilo hakupatikana. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu haukujibiwa.
Mwenyekiti wa CHADEMA jana aliiambia Sauti ya Amerika kuwa tukio hilo lina viashiria vya kisiasa.
Hatuwezi kuamini hili ni tukio la ujambazi. Kama lingekuwa tukio la ujambazi wangebeba kila kitu. Tukio liliotokea watu waliojitokeza na silaha walikuwa wanajiamini, wakiwa na silaha ya SMG, silaha ya kivita, silaha ya moto. Wamefanya mashambulizi wakati wa mchana, hakuna majambazi wanaokwenda katika tukio kwa namna hiyo,” alieleza Mbowe akiwa nchini Kenya.
Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 na 32 zilizolenga mlango wa abiria wa gari lake aina ya Toyota Land Cruiser alikokuwa amekaa, huku risasi tano zikipiga mwilini.
Makamu mwenyekiti wa CHADEMA, Profesa Abdallah Safari ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa hali ya mbunge huyo inazidi kuimarika.

Maoni