Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad, ameeleza maendeleo ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema), baada ya kumtembelea hospitalini Nairobi, Kenya.
Akihojiwa na Redio ya Idhaa ya Kiswahili Deutsche Welle (DW) ya
Ujerumani jana, Maalim Seif alisema Lissu anaendelea vizuri na hajapoteza
mwelekeo.
Jana (juzi) nilimtembelea Lissu na nilipata moyo sana, kwa kweli
anaendelea vizuri ukizingatia mtu ambaye alipigwa risasi zaidi ya 30, anapata
nafuu haraka haraka.
Bado hajapoteza mwelekeo akili yake ipo timamu, ametuhakikishia
haya yaliyotokea hayatamrudisha nyuma katika kuwatetea wanyonge.
Anazungumza vizuri, yuko makini sana anajua anachokisema na mimi
nimepata moyo jinsi nilivyomuona,” alisema Maalim Seif.
Alisema kutokana na mambo yanayoendelea nchini, lazima kuwapo na
mjadala wa taifa kuona tumekosea wapi na kujirekebisha.
“Mambo kama haya kutokea Tanzania ni jambo ambalo kila Mtanzania
lazima aingiwe na wasiwasi kwa sababu hakuna hata mmoja na hasa mwanasiasa
ambaye ana usalama wa maisha yake.
Kama taifa tuzungumze kuona tumekosea wapi na kujirekebisha,”
alisema.
Kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, alisema hata kama vyombo vya
dola vya ndani vitafanya si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine.
Yako mambo mengine yaliyotokea huko nyuma na bado hatujaaambiwa
yalikwenda vipi, tunaambiwa tu uchunguzi unaendelea. Ni vizuri wananchi waone
matokeo ya uchunguzi huo…si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine,”
alisema.
Lissu alipigwa risasi zinazokadiriwa kufikia 32, Septemba
7, mwaka huu, alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma baada ya
kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za
mwili wake.
Maoni
Chapisha Maoni