MAGUFULI AKIGOMBEA URAIS 2020 HAWEZI KUSHINDA.

John Pombe Magufuli, Kama atagombea tena Urais mwaka 2020, hawezi kushinda kwenye uchaguzi ulio huru, haki na uwazi. Mhariri wa gazeti lililofungiwa karibuni la Raia Mwema alipata kuandika kwenye safu yake, kwamba uchaguzi wa mwaka 2020 utaamuliwa na ajenda mbili kuu za msingi, HAKI na UCHUMI. Uchambuzi ambao nakubaliana nao.
Haki: Magufuli anaongoza utawala unaovunja haki za watu kwa kiwango kikubwa sana ambacho hakijawahi kuonekana nchini. Machozi ya wanaovunjiwa nyumba bila fidia (tena kukiwa na zuio la mahakama), watu wanaouwawa hovyo, watu wanaoshambuliwa hovyo kwa mawazo yao tu dhi ya Serikali, watu wanaosekwa ndani kwenye magereza bila makosa, tabia ya visasi dhidi ya watu aliogombana nao kabla hajawa Rais, na uvunjifu wa haki nyengine za kikatiba kama uhuru wa mawazo, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kufanya shughuli za siasa, haki ya kupata Katiba mpya na Haki za Wazanzibari Kwa muktadha wa uchaguzi wa Mwaka 2015.
Hiyo ni mifano michache tu ya ubinywaji wa haki kinyume kabisa na Katiba ya nchi yetu, Katiba ambayo Rais aliapa kuilinda. Wananchi mwaka 2020 hawawezi kumchagua mvunja haki namna hiyo.
Uchumi: Licha ya takwimu kuonyesha kasi ya ukuaji wa uchumi kuwa kubwa kwa kiwango cha 7%, wachumi wanajua kuwa shughuli za uchumi zimedorora na hicho kiwango ni maendeleo ya sera za awamu ya nne ambayo sasa yanakatika.
Tayari makadirio ya kasi ya ukuaji wa uchumi yameshushwa mpaka 6% mwaka 2017 na 5% mwaka 2018. Ikifika mwaka 2020 kasi ya ukuaji wa uchumi itakuwa karibu sawa na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu (2%) na hapo ndio tutaona ongezeko la familia zinazolala bila kula, matumizi ya bidhaa kushuka na mdororo wa uchumi kushika kasi.
Tayari Hivi sasa hali ya maisha imekuwa ngumu kwa wananchi, mauzo ya bidhaa za viwanda nje kwaajili ya fedha za kigeni yameshuka kwa zaidi ya nusu, malipo yetu nje yamekuwa na urari hasi kwa sababu ya maamuzi ya hovyo ya miradi mikubwa kama ndege na Reli (miradi muhimu iliyotekelezwa bila weledi wa maarifa ya uchumi wa dunia unavyoendeshwa).
Sekta ya Kilimo imeshuka mpaka kiwango cha kabla ya Uhuru, kwani kasi ya ukuaji wa sekta ya Kilimo mwaka 2016 ilikuwa 1.6% tu. Wakulima wa Korosho hawajapewa pembejeo, hivyo uzalishaji wa zao linalotuingia mapato ya Kigeni zaidi nchini utashuka msimu huu wa mavuno, Tumbaku (zao la pili Kwa kuingiza Fedha za kigeni) tayari wakulima wanalia, mazao ya choroko na kunde bei imeshuka kwa zaidi ya 500%, Pamba uzalishaji umeshuka Kwa 63% kati ya mwaka 2015 na 2017 (miaka miwili ya Magufuli), na mauzo Nje ya dhahabu kuanza kushuka na hivyo kupelekea shilingi kushuka thamani na hivyo mfumuko wa bei kupanda Kwa kasi.
Kutokana na shughuli za Uchumi kudorora, Mapato ya Serikali Kwa mwezi yameanza kushuka kufikia chini ya makusanyo aliyoacha Rais wa Awamu ya Nne. Mtu anayeangusha uchumi kwa kasi ya namna hiyo anawezaje kuchaguliwa tena na Watanzania kuwa Rais?
Kuna njia 2 tu za kumfanya John Pombe Magufuli kuwa Rais baada ya mwaka 2020, nazo ni zifuatazo:
1. Muswada wa Mabadiliko ya Katiba wa Mbunge Juma Nkamia ili kuongeza muda wa kukaa madarakani kutoka miaka Mitano ya saaa mpaka miaka 7.
2. Vyama vya Upinzani na Jumuiya za Wananchi kushindwa kuweka Mgombea mmoja wa kushindana naye.
Nje ya hapo Magufuli hana nafasi ya kuwa Rais 2020. Niwaase wananchi wenzangu, tunayo nafasi nzuri zaidi ya kung'oa utawala uliochoka wa CCM mwaka 2020 kuliko wakati wowote ule.
Komredi Ado Shaibu

Maoni