MEYA LAZARO AMEKUWA NA USHAWISHI MKUBWA ALAT NA UJASIRI ILA MWENYEKITI WA ALAT KAJAWA UWOGA.

Meya wa Jiji la Arusha azua Gumzo Alat.
HOTUBA ya Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli imezua mjadala mzito kwenye Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) baada ya baadhi ya wajumbe kutaka ijadiliwe.
Ni baada ya Rais Dkt. Magufuli kuhutubia mkutano huo juzi (Okt. 3) ulioanza Oktoba 2 hadi 5, 2017, na unafanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JKICC) jijini Dar es Salaam.
Meya wa Jiji la Arusha Kalisti Lazaro ndiyo aliwasilisha hoja hiyo jana (Okt. 4) kwenye siku ya tatu ya mkutano huo kwa Mwenyekiti wa ALAT Taifa Abubakar Mukaddam, ambapo alisema hotuba ya Rais imesheheni mambo mengi, hivyo haiwezi kupita bila kujadiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana (juzi) Rais wetu alitoa hotuba iliyojaa vitu vingi vinavyogusa halmashauri zetu. Katika hali ya kawaida, hatuwezi kukaa na kuanza kujadili taarifa za taasisi za Serikali na kuacha kujadili hotuba ya Rais. Naomba tuache shughuli zote tujadili hotuba hiyo" alisema Lazaro.
Meya huyo ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa hapa jijini Dar kwa hoja nzito alimtaka mkiti wa ALAT Taifa kuwa kuna maswala lazima yajadiliwe kwani hata Rais alitaka tujadili na kumpelekea maazimio hivyo kuzuia kujadili ni kutoitendea haki hotuba na Rais mwenyewe.Kuna mambo ya posho za madiwani ambapo diwani analipwa laki tatu na elfu hamsini kwa mwezi na wenyeviti wengi wakiambulia elfu hamsini kwa mwezi jambo ambalo halina uwiano na majukumu yao,misharahara ya watumishi ambapo alisema jiji la Arusha yenyewe ina watumishi zaidi ya 4000 hivyo kutoongezewa nyongeza ni kuwavunja moyo na morali,tuna madeni ya wakandarasi kwenye miradi inayotegemea ruzuku,ulinzi wa raslimali kama misitu,Madini,wanyamapori,mafisadi,matumizi ya raslimali kunufaisha umma,hoja ya viwanda ,Hivyo hotuba hii ikijadiliwa itaweka mwelekeo mpya na kumsaidia Rais kwa kazi ya kusimamia raslimali ya nchi yetu.Kukataa kujadili ni kumdhalilisha Rais na kumwonyesha amekuja kupoteza muda na nguvu zake mbele yetu,ama kuonyesha hatumwamini Rais na maneno yake ,hata hivyo wajumbe walimwunga mkono ila meza kuu akiwemo Mkiti wa ALAT akielekeza ni maagizo toka juu kutojadili hotuba hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Jenifa Omollo alisema hotuba hiyo haiwezi kujadiliwa kwa vile ni maagizo na maelekezo, hivyo kama kuna mtu anataka kuijadili aende akafanye hivyo kwenye halmashauri yake kwa ajili ya utekelezaji.
Hotuba ya Rais haiwezi kujadiliwa kwa vile hayo ni maagizo na utekelezaji, hivyo hata kama tutajadili hapa hatutapata muafaka kwa vile kila halmashauri ina changamoto zake, hivyo kama kuna mtu anataka kujadili hotuba hiyo anatakiwa aende kwenye halmashauri yake na kuona ni jambo gani kwake atalipa kipaumbele" alisema Omollo.
Mwenyekiti wa ALAT Taifa Mukkadam alipinga hotuba hiyo kujadiliwa, kwani watakuwa wanapingana na Rais, na kutaka wajumbe wawe na uelewa na kutofautisha chombo cha ALAT na Bunge, ni baada ya baadhi ya wajumbe kudai mbona Rais akihutubia Bunge, hotuba yake inajadiliwa.
Hatuwezi kujadili hotuba ya Rais, huko ni kumkosea adabu. Hatuwezi kukaa hapa na kupambana na mamlaka ya Rais. Sisi tunachotakiwa ni kuipokea na kwenda kuifanyia kazi" alisema Mukkadam.
Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Abdallah Ngodu alisema taarifa alizozipata mchana wa jana (Okt. 4) kutoka Ikulu ni kuwa Rais atatoa nakala ya hotuba yake kwa kila halmashauri ili kuwa na kumbukumbu na kuweza kufanyia kazi hotuba hiyo kwa utekelezaji.
Akihutubia juzi (Okt. 3) wajumbe wa ALAT, Rais Dkt. Magufuli alisema watumishi hewa wamechangia kudumaza huduma za kijamii na miradi ya maendeleo kutokana na fedha hizo kulipwa kwa watu ambao hawakustahili.
Alisema watumishi hewa hao hawakuja kwa bahati mbaya, bali kulikuwa kuna wajanja wachache ndani ya mfumo wa Serikali ambao walikuwa wananufaika na hilo.
Rais Dkt.Magufuli alisema pamoja na watumishi hewa pia kulikuwa na wenye vyeti vya kughushi, ambao kwa namna moja ama nyingine, nao walikuwa wanapata mishahara wasiyostahili, lakini pia wamesababisha watu kupuuza kujiendeleza kielimu, kwani walikuwa na uhakika wa kupata pesa.
"Watumishi hewa 20,000 kwa mwezi walikuwa wanalipwa sh. bilioni 19.8, hivyo kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 238.1. Hawa watu hawakuwa kwenye vitabu, lakini kila mmoja alikuwa na mtu wake serikalini anamlinda.
Pesa hizi ni nyingi, na zingeweza kulipa posho madiwani, kujenga vyoo vya wanafunzi wetu, kununua dawa ama kujenga nyumba za walimu. Lakini kuna watu walikuwa wanalipana fedha hizo, kwangu ni kama kuzitupa chooni" alisema Dkt. Magufuli.
Dkt. Magufuli alisema mishahara hewa ilikuwa inaendana na likizo za uzazi hewa, likizo za kawaida hewa na pensheni hewa, hivyo kuagiza fedha za pensheni sh. bilioni 38 zilizolipwa kama pensheni kwa watumishi hewa, zirudishwe serikalini.
Alisema mapambano hayakuwa kwenye watumishi hewa tu, kwani wenye vyeti vya kughushi zaidi ya 12,000 walikuwa wanalipwa sh. bilioni 11.9 kwa mwezi, na kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 142.9 kwa mwaka.
"Hivyo wafanyakazi hewa 20,000 na wenye vyeti vya kutengeneza Kariakoo 12,000 wote kwa mwaka walikuwa wanalipwa sh. bilioni 381. Hawa wote walikuwa wanazorotesha ufanisi na kuondoa ari ya kuwajibika. Lakini wenye haki walikuwa hawapati fursa" alisema Dkt. Magufuli.
Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli alikataa ombi la ALAT la kutaka madiwani waongezewe posho kutoka sh. 350,000 kwa mwezi hadi sh. 800,000, na kusema kwa sasa tujenge nchi kwanza na posho zitafuata baadae, kwani anaamini mtu anaeomba udiwani ana shughuli ya kufanya.





Maoni