VICHWA VYA TRENI VIMEANDIKWA TRL ILA SERIKALI INASEMA MUHUSIKA WA VICHWA AONEKANI JE?TRL NI NANI?


 
Serikali imesema ipo katika mchakato wa kuvinunua vichwa 13 vya treni ambavyo vilitelekezwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo jana Ijumaa wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa mashine za ukaguzi wa mizigo(Scanners) zenye thamani ya Sh27 bilioni kwa ajili ya kuongeza ulinzi na udhibiti wa mapato kwenye bandari hiyo.


Profesa Mbarawa alisema Serikali imeunda timu ya wataalamu 11 kwa ajili ya kufanya tathmini ya ubora pamoja na thamani ya fedha ya vichwa hivyo na baada ya kukamilika watafanya makubaliano na mmiliki wa vichwa hivyo ili kuvinunua.


Julai mwaka huu katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwaajili ya upanuzi wa bandari hiyo Rais John Magufuli alisema ana taarifa ya vichwa vya treni vilivyoshushwa bandarini hapo lakini mmiliki wake hajulikani huku akisisitiza kuwapo kwa mchezo mchafu.


Utata huo uliibuka kufuatia Shirika la Reli Tanzania(TRL) kununua vichwa hivyo kupitia mkataba wake na kampuni ya EMD ya Marekani na utengenezaji ukafanywa na kampuni ya DCD ya Afrika Kusini huku taratibu za ununuzi zikidaiwa kukiukwa.


Hata hivyo tayari Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alishaeleza kuwa vichwa hivyo vina nembo ya TRL lakini vilizua mgogoro baada ya kubainika kuwa mchakato wa ununuzi haukuwa sahihi.


Lakini kwa mujibu wa taarifa iliyowahi kutolewa kwa vyombo vya habari na TRL Machi 23, 2015 ilibainisha kuwa vichwa viwili kati ya 15 vya treni vilivyonunuliwa na shirika hilo vilipokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam Machi 21, 2015.


Taarifa hiyo ilisema vichwa hivyo vimetengenezwa nchini Afrika Kusini na kwamba ununuzi huo umegharimu kiasi cha Sh70.9 bilioni ambazo zote zilishalipwa.

Maoni