APATA HUKUMU YA MAISHA KWA KOSA LA KUMBAKA MTOTO.

 

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu, Peter Ngomalala (50) mkazi wa Kijiji cha Sibwesa katika Wilaya ya Tanganyikakifungo cha maisha baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa alisoma hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Flavian Shiyo uliwaita mashahidi kadhaa akiwemo mtoto huyo aliyebakwa na pia mama yake mzazi. Hakimu alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha Sheria namba 130 (1)(2) na kifungu cha Sheria 131 (3) kanuni ya adhabu.

Amesema mtoto mwingine aliyeshuhudia na aliyebakwa wote pamoja na kuwa na umri mdogo, bado walitoa ushahidi kwa ufasaha ambao haukuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

 

Hakimu amesema mahakama hiyo ilijiridhisha na ushahidi wa muuguzi wa zahanati ya Sibwesa mtoto huyo alikofanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kupewa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs).

Awali Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Shiyo alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 12, 2016 saa 4 asubuhi kijijini Sibwesa ambapo alimkuta mtoto huyo akicheza na mwenzake jirani na kwao akawalaghai watoto hao wamfuate nyumbani kwake akawape fedha wanunue biskuti na vinywaji baridi.

Maoni