BAADA ya kutenda mema, wakasema ASULUBIWE! Na LazaroNyalandu
NIMEINGIA Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uteuzi wa Rais Jakaya
Kikwete, Mnamo Februari 10, 2014, na nimefanya kazi ya Uwaziri kwa
takribani miezi 18.
Itakubukwa kwamba kipindi hiki kilikuwa ni
kilele cha ujangili wa Tembo barani Afrika, huku Tanzania ikitajwa kuwa
nchi kinara kwa masuala ya ujangili wa wanyamapori, hususani Tembo.
Wakati huo, akiba ya meno ya Tembo katika Ghala la Taifa yalifikia
takribani tani 130,000, ikiwa ni idadi kubwa ya meno ya Tembo
yaliyohifadhiwa popote duniani.
Kazi yangu ya kwanza ilikuwa ni
kuongozana na Rais Jakaya Kikwete kwenda London, Uingereza kuhudhuria
Mkutano wa Tembo duniani ulioandaliwa na Mwana Mfalme Charles wa
Uingereza, ambako pamoja na mambo mengine, Rais Jakaya Kikwete
aliitaarifu dunia juu ya uamuzi wa Tanzania wa kupiga marufuku biashara
ya meno ya Tembo, na kuungana na Mataifa lukuki yaliyokubali kufanya
hivyo.
Aidha, kwa kushirikiana na Rais Jakaya Kikwete,
tulikubali Tanzania kujiunga na Mataifa 6 barani Afrika (African
Elephants Range States), ikiwepo Ethiopia, Kenya, Gabon, Chad, Botswana
na mataifa mengine kwa lengo la kuongoza mapambano hayo. Mara baada ya
Mkutano wa London, Tanzania na baadhi ya Mataifa ya Afrika yalikuwa
washiriki wa Pound milioni 10 zilizotolewa na UINGEREZA kupambana na
uhalifu huo Afrika. Niliporejea Tanzania, nilianzisha Mpango wa
Kuhifadhi Vema Akiba ya Meno ya Tembo nchini kwa kuyafanyia utambuzi wa
DNA (asili, umri wa Tembo, na alikotokea) na kuhakikisha hayapotei, kazi
iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya watalaamu wa Wizara na Shirika la
STOP IVORY UK.
Aidha, kama Waziri, kwa idhini ya Rais, nilihojiwa
na Stephen Sucker wa kipindi maarufu Cha BBC HardTalk, nikiwa Mtanzania
wa Pili wakati huo kuhojiwa HardTalk, wa kwanza akiwa Rais Mstaafu
Benjamin William MKAPA, na nilipata fursa ya kuielezea dunia azma ya
Tanzania kuongoza mapambano dhidi ya Ujangili barani Afrika.
Kwa
kuzingatia changamoto waliyokuwa nayo wahifadhi kote nchini,
niliiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kufanya mchakato wa
kuongeza idadi ya Maaskari wa Wanyamapori kutoka 1000 hadi 4000, na
kuanzisha mazoezi mahsusi kwa Maaskari wa Wanyamapori katika Pori la
Akiba la Selous kwa kushiriana wa kikosi Maalum Cha US Special Forces
kilichopo mjini Stuttgart, Ujerumani. Maaskari wa Wanyamapori
walifundishwa umahiri na weledi katika kufanya kazi yao, na walipatiwa,
kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, vifaa vya kuwawezesha kumudu
hali yenye changamoto wanapokuwa porini. Aidha, Serikali ya Ujerumani
ilikubali kutoa Uniforms na boots kwa ajili ya Askari wetu, ikiwa ni
hatua za awali za kuwajengea morali na utayari wa kuitumikia nchi
wanapokuwa katika mazingira tete porini.
Wakati huo huo, Taasisi
ya Howard Buffet Foundation ilikubali kutoa helikopta kwa ajili ya
Doria, Shirika la FZS walitoa ndege yenye kamera maalumu (infra red),
Friedkin Conservation walikubali kutoa helikopta, Kilimanjaro Safari
Club walitoa ndege, na Mkuju River Project walitoa ndege. Ndege ya FZS
ilikuwa na kamera maalumu (infra red) zinazoweza kuwatambua majangili
porini nyakati za usiku. Taasisi ya HBF, ilitoa fedha, magari, pamoja na
kukikarabati Chuo Cha Maaskari wa Wanyamapori Pansiasi Mwanza na
kununua vitendea kazi vingine kwa ajili ya maaskari wanafunzi.
Tukiwa tumeongeza idadi ya wapiganaji, nilishirikiana na Taasisi ya Paul
Allen (mwanzishi mwenza wa Microsoft) kuidadi (kuhesabu) upya Tembo
nchi nzima, ambako baada ya mwaka moja, idadi ya Tembo ikaanza
kuongezeka sana kutokana na jitihada hizi shirikishi. Aidha, kupitia
Paul Allen, tulianzisha mfumo mpya wa mawasiliano Selous uitwao Digital
VHS, wenye lengo la kuwawezesha Maaskari kuwa na mawasiliano
yasiyoingiliwa kimtandao na majangili na watu wengine wenye nia mbaya.
Halikadhalika, kwa kuzingatia hali tete ya kupotea kwa Tembo katika
hifadhi ya Ruaha wakati huo, nilishirikiana na Serikali ya Marekani
kupitia Taasisi ya WCS (World Conservation Society) yenye Makao yake
Makuu mjini New York, ambayo ilianzisha mradi wa muda mrefu wa dola
milioni 50 kuokoa Hifadhi ya Ruaha pamoja na maeneo mengine.
Mwaka huo huo, kwa kushirikiana na Shirika la International Conservation
Caucus (ICCF) la Mjini Washington, DC, pamoja na Shirika la Umoja wa
Mataifa UNDP-Tanzania na Benki ya Dunia, (ofisi ya Tanzania) niliitisha
Mkutano wa Nchi 11 za Africa uliofanyika mjiini Arusha, na kukubaliana
juu ya Azimio la Arusha “Arusha Declaration” kuhusu kushirikiana
kuhifadhi maeneo yanayoingilina (shares ecosystems) katika nchi zetu.
Washiriki wa Maendeleo ikiwepo Ujerumani, UNDP, na Marekani walishiriki
nami katika kutia sahihi makubaliano kati ya Tanzania na Msumbiji
(Selous-Niassa Corridor Agreement) tuliyoyafikia mjini Maputo, Msumbiji
kuhusu kulinda ushoroba wa Selous-Niassa kati ya Msumbiji na Tanzania
unaokadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 40,000, ukiwa ni
ushoroba mkubwa kuliko zote duniani.
Nilichukua hatua ya
kuzishauri na kukubaliana na nchi zenye misitu ya asili ‘miombo
woodland’ ambayo ndio misitu ya asili kwa Hifadhi ya Tembo barani Afrika
zikubali kutia saini “Miombo Woodland Agreement”, ikiwa ni sehemu ya
jitihada za mataifa haya kuhifadhi Tembo, na uoto wa asili wa Miombo,
ambao unasaidia pia kuzuia mabadiliko ya tabia nchi duniani. Nchi
zilizokubali ni pamoja na Zambia, Malawi, na Msumbiji, na tulianza hatua
za awali za kufanya jitihadi za nchi hizi zijulikane na kutambuliwa na
Umoja wa Mataifa Wakati wa Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, Paris,
Ufaransa. Tanzania na Zambia zilikuwa nchi za kwanza kuweka sahihi
Makubaliano hayo.
Nilianza mchakato na Benki ya Dunia wa kutoa
dola 150, 000,000 kwa ajili ya kusaidia kuinua Utalii kusini mwa
Tanzania (mikoa ya kusini mwa reli ya kati), pia tulipata Euro milioni
50 kutoka Ujerumani kwa ajili ya kusaidia Uhifadhi kupitia uanzishwaji
wa TAWA, na Serikali ya China ilitoa magari mapya na pikipiki maalumu za
matairi matatu kwa gharama ya zaidi ya dola milioni Moja na nusu.
Aidha, kwa ushirikiano Mkubwa na wenzangu Wizarani, Nilifanikisha
kuanzisha Taasisi Mpya kabisa Tanzania ya TAWA (Tanzania Wildlife
Authority), inayochukua kazi za kiuhifadhi za idara ya Wanyamapori.
Nilishirikiana na wenzangu Wizarani kuandaa mfumo wa uendeshaji wa
taasisi hii ili iweze kuwa kinara Cha Uhifadhi nchini kwa kumiliki na
kulinda mapori yote ya Akina (Game Reserves), Mapori Tengefu, na maeneo
yote ya Wanyamapori yaliyo NJE ya uangalizi wa Tanapa au Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro. Serikali ya Ujerumani, kama nilivyosema hapo
awali, ilitoa Euro milioni 50, na Serikali ya Tanzania ilikubali Shirika
hili la Umma liwe na Makao yake Makuu Mjini Morogoro.
Baada ya
kuleta helikopta Wizarani, nilianzisha mpango maalumu wa kuwafundisha
vijana wa Kitanzania mafunzo ya urubani wa Helikopta na ndege nchini
Afrika Kusini na Marekani, na tayari kuna vijana waliofuzu vema.
Pamoja na kwamba siwezi kuyaeleza yote kwa sasa, ikumbukwe kuwa
nilianzisha Tangazo la “Tanzania, the Soul of Africa”, nilianzisha
Swahili Expo kwa ushirikiano na Indaba SA, na tulifanikiwa kwa
ushirikiano na wadau wa Utalii nchini, kuongeza idadi ya watalii kuvuka
milioni na pato la Utalii kufikia dola bilioni 1.3, huku Benki Kuu
Tanzania ikiarifu kuwa Sekta ya Utalii wakati huo ilikuwa inaongoza kwa
kuingiza nchini Fedha za kigeni, forex.
HIZI ni baadhi ya KAZI nilizozifanya ndani ya miezi 18 nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Waziri Kigwangalla pamoja na wale waliopania kuniumiza wanahitaji
miwani yenye lensi za ziada yamkini kwamba, macho yao yaweze kuona, na
ndimi zao ziweze kukiri mema haya ambayo MUNGU alitujalia kuyafanya kwa
pamoja nikiwa Waziri wa Maliasili. Iliandikwa zamani, “Kama hamniamini
mimi, basi aminini kazi ninazozifanya”. Miaka zaidi ya miwili baada ya
mimi kumaliza kazi yangu ya uwaziri nikiwa salama, na baada ya kuhama
CCM, wamenigeuza adui. Katika Wizara ya Maliasili, Mimi Nyalandu
sikuwahi kufukuzwa, kuachishwa, wala kutumbuliwa muda WOTE nikiwa
Wizarani, ikiwa ni historia kubwa ikizingatiwa kuwa Mawaziri wengi
hawakumaliza Salama. Mwenye masikio na ayasikie maneno haya. MUNGU
awakemee wote wanaokaa vikao vya SIRI kupanga hila juu yangu, MUNGU
akalikomboe Taifa letu dhidi ya roho ya HOFU inayofanya wengi kunyamaza
huku wakiona Taifa linaangamia, ikawe HERI kwa wote waitamanio HAKI, na
ni maombi yangu kwamba MUNGU afufue UJASIRI, na afufue KAZI yake
katikati ya MIAKA. Taifa Tanzania na watu wake watasimama TENA.
Tushikane MIKONO. Tuamini. Tuungane.
SIGNED
Lazaro S. Nyalandu.
Waziri Mstaafu, Maliasili na Utalii, Tanzania
Maoni
Chapisha Maoni