Ruka hadi kwenye maudhui makuu
LHRC KIMEBAINI UVUNJIFU MKUBWA WA HAKI ZA BINADAMU PAMOJA NA TARATIBU ZINAZOSIMAMIA UCHAGUZI NCHINI TANZANIA
KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU(LHRC) Justice Lugakingira House, Kijitonyama, P. O. Box 75254, Dar Es Salaam, TANZANIA
Telephone: 2773048, 2773038, Fax: 2773037, E-mail: lhrc@humanrights.or.tz
Website www.humanrights.or.tz
TATHMINI YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA
MADIWANI WA MARUDIO WA 26 NOVEMBA, 2017 ULIOFANYIKA KATIKA KATA 43.
Tarehe: 28 Novemba 2017
Awali ya yote, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ni Shirika
lisilo la kiserikali, la kujitolea, na lisilo la kisiasa, wala si la
kutafuta faida binafsi. Shirika limejikita katika kulinda, kutetea na
kuimarisha Haki za Binadamu na Utawala Bora katika nchi, ili kufikia
kuwa na jamii yenye Haki na Usawa.
Kituo kimefuatilia kwa karibu
uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani katika kata 43 zilizopo
halmashauri takribani 36 kwenye mikoa 19 nchini Tanzania uliofanyika
tarehe 26 Novemba 2017, kupitia waangalizi wetu wa haki za binadamu
(Human Rights Monitors) na kupata taarifa kwa njia mbalimbali za vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii. Ifahamike kwamba Uchaguzi huu
umefanyika ili kujaza nafasi zilizo wazi katika kata hizo baada ya
madiwani waliokuepo, kufariki, kujiuzuru na wengine uwakilishi wao
kutenguliwa na mahakama.
Pamoja na ukweli kwamba, baadhi ya kata
Uchaguzi umefanyika kwa uhuru na haki lakini Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kimebaini uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu pamoja na
taratibu zinazosimamia uchaguzi nchini Tanzania. Kumekuwa na vitendo
vya matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa
na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa kwa lengo
la kuharibu na kuvuruga uchaguzi na vile vile kuwatia hofu wapiga kura,
Vitendo hivi vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu
wasiojulikana na watu wanaosadikika kuwa wafuasi wa vyama vya siasa
ikiwemo Chama Tawala (Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) na vyama vingine vya upindanzani kama taarifa
yetu itavyofafanua kwa kina.
Kutekwa, kukamatwa, kupigwa na kujeruhiwa Viongozi wa Vyama na wapiga kura.
Utekwaji; Imeripotiwa kwamba, kuna matukio ya kukamatwa na kutekwa kwa
watu katika kata ya Kitwiru, Iringa mjini na Vijana wanaosadikika kuwa
ni kikosi cha ulinzi cha CCM maarufu kwa jina la Green Guard,
waliwavamia na kuwateka wanachama wanao semekana ni wa CHADEMA, ndg.
Eliza Nyenza na ndugu, Martha Francis walipokuwa wakienda kupiga kura,
kisha kunyang’anywa simu na kuwatelekeza katika msitu wa Kilolo hadi
walipopata msaada wa wapita njia. Vile vile kushambuliwa kwa gari la
Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Mh.Daddy Igogo, huku Jeshi la Polisi
likimkamata na kumshikilia Meya wa Manispaa hiyo, Mh. Alex Kimbe.
Pia kuna matukio yameripotiwa kuhusu kupigwa na kujeruhiwa kwa mawakala
na wanachama wa Vyama vya siasa. Imeripotiwa kuwa Mfuasi wa CCM katika
jimbo la kawe, alivamiwa na kujeruhiwa na watu wanaosadikika ni wafuasi
wa chama cha CHADEMA, hatimaye kulazwa katika Hospitali ya Rabinisia,
Tegeta jijini Dar es Salaam. Kama inavyoonekana katika picha hapo chini .
Katika Kata ya Makiba, wakala wa CHADEMA ndg. Rashid Jumanne na
Mwenyekiti wa CHADEMA Tawi la Valeska, ndg. Nickson Mbise wamejeruhiwa
vibaya baada ya kushambuliwa kwa mapanga mapema asubuhi walipokuwa
wakielekea katika vituo vya kupigia kura.
Iliripotiwa kwamba,
katibu wa CCM Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu akiwa amelazwa hospitalini
baada ya kushambuliwa na watu wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa CHADEMA
wakati akiwasindikiza mawakala wa Chama chake kwenda vituoni kwa ajili
ya kusimamia kura. Kama kielelezo hapo chini kinavyojieleza.
Vitendo hivyo pia vimeripotiwa katika kata za Nyabubhinza, Maswa na
Simiyu, Mawakala katika vituo nane (8) kati ya vituo 13 walikamatwa na
Jeshi la Polisi ikiwemo Diwani wa CHADEMA ndg. Zakayo Chacha Wangwe.
Pia, katika kata ya Kimweri wilayani Meatu ndg, Emmanuel Nawadi akiwa na
mawakala wawili wakielekea kwenye vituo vyao majira ya alfajiri,
walivamiwa na kushambuliwa na vijana wanaosadikika wanachama wa CCM
ambapo diwani huyo alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa na mapanga.
Kuna
matukio yameripotiwa kuhusu Viongozi wa vyama vya siasa na mawakala wa
vyama kukamatwa mathalani Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Ubungo ambaye
alikuwa mratibu mkuu wa uchaguzi wa Kata ya Saranga, ndugu, Perfect
Mwasiwelwa, alikamatwa na Jeshi la Polisi tangu 25.11.2017, imeripotiwa
kwamba jeshi la polisi limemkamata meya wa Ubungo na Mwenyekiti wa
CHADEMA Wilaya ya Ubungo, Mh. Boniface Jacob siku ya Uchaguzi ambaye pia
ndiye aliyeapishwa kuwa Wakala Mkuu kwenye majumuisho ya kura za mwisho
katika Kata.
Katika tukio lingine, imeripotiwa kwamba Mgombea
Udiwani kwa tiketi ya CHADEMA kata ya Sofi, wilaya ya Malinyi Mkoani
Morogoro. Ndg. Rico Venance alikamatwa akiwa anatembelea vituo
mbalimbali vya kupigia kura ambapo ni haki yake kwa mujibu wa taratibu
zinazosimamia uchaguzi. Jeshi la polisi halijasema hadi sasa sababu za
msingi za kuwakamata na kuwashikilia mawakala na Viongozi hawa wa
kisiasa.
Imeripotiwa pia, mawakala wote wa CHADEMA katika Vituo
takribani 13, Kata ya Mamba, Wilaya ya Bumbuli na Tanga, Waliondolewa
katika vituo vyao majira ya saa nne asubuhi siku ya Uchaguzi na
kupelekwa kituo cha Polisi na hakuna sababu iliyotolewa ya kukamatwa
kwao. Lakini vile vile Kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA
katika Kata ya Ibighi, wilaya ya Rungwe na Jeshi la Polisi bila sababu
yoyote kutolewa. Imeripotiwa Waliokamatwa ni ndg George Tito, Award
Kalonga na Wenzake.
Mawakala kutolewa katika Vituo Vya Kupigia kura Arusha.
Ni takribani kata 6 za jimbo la Arumeru Mashariki, kata ya Ngabobo,
Makiba, Leguruki, Ambureni, Maroroni na Musa, mawakala wote walitolewa
nje ya Vituo vya kupigia kura huku zoezi la upigaji kura likiendelea
ndani. Sababu za kutolewa nje ni fomu za mawakala za viapo vya
kuwatambulisha kusainiwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi badala ya
Msimamizi wa Uchaguzi jimbo. Baada ya masaa takribani manne (4),
mawakala wote wa vyama vya siasa waliamriwa kurejea ndani ya vituo.
Mazingira haya yana viashiria vya kuufanya uchaguzi usio huru na haki
kwani wagombea walikosa haki yao ya kisheria ya kuwakilishwa na
mawakala.
Aidha kuna matukio yameripotiwa juu ya mawakala wa CHADEMA
kuzuiliwa kuingia ndani ya vituo katika Kata ya Saranga, Manispaa ya
Ubungo, jimbo la kibamba na hivyo kuchelewa kwa takribani saa zima, huku
uchaguzi ukiwa unaendelea ndani, kwa sababu Msimamizi wa Uchaguzi wa
Jimbo la Kibamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, ndg,
John Kayombo, alikuwa amewanyima barua/fomu zao za kuwatambulisha kama
mawakala vituoni. Baada ya nguvu ya umma kutumika ndipo wakaruhusiwa
kuingia vituoni kwa kuchelewa.
Kutokana na Matukio haya ya uvunjifu
wa haki za binadamu pamoja na mwenendo mzima wa uchaguzi katika baadhi
ya kata tajwa hapo juu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaona
matendo haya si mazuri, na yana viashiria vyote vya kukandamiza
demokrasia nchini Tanzania. Vile vile, kuna hatari ya kukuza utamaduni
wa kulipizana visasi kwa chuki za kisiasa kitu ambacho kitapelekea
uvunjifu wa amani kama taarifa hii inavyojieleza.
Kituo kinaomba
serikali pamoja na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua
hatua kali za kisheria kwa wote watakao bainika kuhusika kwa namna moja
au nyingine katika uvunjifu huu wa haki za binadamu na uvurugaji wa
uchaguzi. Pia kituo kinatahadharisha kwamba matukio haya yasipokemewa na
jamii nzima ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakao athiri chaguzi
zijazo ikiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi
mkuu wa Mwaka 2020 kwa kuogofya wapiga kura wasijitokeze kutekeleza haki
zao za msingi za kuchagua viongozi wao, kuchochea uhasama miongoni mwa
wananchi na wadau wengine wa uchaguzi pamoja na kufifisha Imani ya
wananchi juu ya Vyombo vya Usimamizi wa Uchaguzi na dola kwa ujumla.
Hapo chini ni picha zinazoonyesha Ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea katika baadhi ya kata.
Tamko limetolewa na ;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
………………………….
Maoni
Chapisha Maoni