MAJIBU YA RAIS WA TANZANIA MAGUFULI KWA WABUNGE WAJENGA HOJA BASHE NA NAPE.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewatumia ujumbe Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kuhusu hoja walizozitoa Bungeni.

Wakichangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2018/2019, wabunge hao walimkosoa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kuwa ameshindwa kumshauri vizuri Rais kuhusu kutumia fedha kutekeleza miradi kama ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa badala ya kutumia wawekezaji.

Baada ya mjadala huo, Dkt. Mpango aliliambia Bunge kuwa alipigiwa simu na Rais Magufuli ambaye alimpa ujumbe awafikishie wabunge hao.

“Naomba ninong’one na Bunge lako tukufu. Mheshiwa Rais Magufuli aliposikia huu mjadala alinipigia simu na aliniambia hivi, ‘Waziri, mwambie ndugu yako mheshimiwa Nape na mheshimiwa Bashe kuwa nawataka sana hao wawekezaji kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway (reli ya kati ya kisasa)’. Hayo ni maneno ya mheshimiwa Rais,” alisema Dkt. Mpango.

 Aliongeza kuwa Rais Magufuli amesema kuwa kama watawaleta hao wawekezaji yuko tayari kuwapa ujenzi wa reli kutoka Kaliua hadi Mpanda au Isaka hadi Mwanza, au reli ya Mtwara hadi Mchuchuma, hadi Liganga ili wajenge.

Waziri Mpango alisisitiza kuwa Serikali inafanya kazi na sekta binafsi lakini changamoto ni pale wawekezaji wanapokuja na masharti ambayo hayatekelezeki au hayana usawa.

Maoni