MWAKA SASA TOKA KUPOTEA BEN SAANANE ILA VYOMBO VYA USALAMA KIMYA TUKUMBUKE MAPAMBANO YA KUMTAFUTA CHINI YA M/KITI WA UTG MALISA.


1. KUPOTEA KWA KATIBU WA UTG NDG.BEN SAANANE.
Ndugu waandishi wa habari,
Mnamo tarehe 18 November mwaka huu (2016), Katibu wa kundi hili Ndugu Benard Focus Saanane au maarufu kama Ben Saanane aliondoka nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, na tangu siku hiyo hajaonekana tena hadi leo yapata siku 24.
Tukio la kupotea kwa Ndugu Saanane lilianza kuibua mijadala kuanzia tarehe 26 November mwaka huu baada ya Ben kutokuonekana nyumbani kwake Tabata, na katika eneo lake la kazi ambalo ni Makao makuu ya chama cha demokrasia na maendeo (CHADEMA).
Baada ya siku kadhaa za kutokujulikana alipo, familia yake ikawasiliana na watu mbalimbali wa karibu na Ben kujua kama wana taarifa yoyote kuhusu Ben alipo. Baada ya kukosa taarifa kuhusu Ben alipo familia ikishirikiana na uongozi wa UTG ilichukua hatua kadhaa kama ifuatavyo:
1. Kutoa taarifa Makao makuu ya Jeshi la Polisi na katika kituo cha Polisi Tabata mnamo siku ya jumatatu ya tarehe 05/12/2016 na kupewa RB namba TBT/RB/8150/2016 ambapo pamoja na mambo mengine Polisi walitoa ruhusa ya kumtafuta Ben maeneo mbalimbali.
2. Jumatatu hiyo ya tarehe 05/12/2016 iliundwa kamati maalumu yenye wajumbe kutoka UTG na baadhi ya wanafamilia na kuanza kumtafuta Ben maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Mahospitalini ambapo ilitembelea hospitali ya Amana, Temeke, Mwananyamala na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kote huko kamati hiyo ilipewa ushirikiano wa kutosha na kukagua vyumba vya wagonjwa mahututi, orodha ya wagonjwa waliolazwa hospitalini humo wasiotambulika (unknown cases) na katika vyumba vya kuhifadhia maiti lakini hakupatikana.
3. Baada ya kumkosa Ben katika hospitali hizo kamati ilitoa mrejesho Polisi na kuomba wawasiliane na vituo vyao ili kujua kama Ben ameshikiliwa mahabusu katika kituo chochote cha Polisi jijini Dar. Polisi waliijibu kuwa Ben hajashikiliwa katika kituo chao chochote jijini Dar.
Kamati iliomba kujiridhisha kwa kupita katika vituo hivyo na kukagua. Kati ya tarehe 6 na 7 mwezi huu kamati ilipita na kukagua mahabusu katika vituo vyote vikubwa vya Polisi jijini Dar vikiwemo Kituo cha Polisi Oysterbay, Mabatini, Urafiki, Magomeni, Buguruni, Chang'ombe na kituo cha Polisi Sitaki shari lakini Be hakupatikana katika vituo hivyo, wala hakuwemo katika orodha ya mahabusu waliowahi kufikishwa katika vituo hivyo.
4. Baada ya hapo kamati ilipata fursa ya kwenda kuuliza katika magereza mawili jijini Dar es Salaam yanayohifadhi Mahabusu, (gereza la Segerea na gereza la Keko) lakini hakupatikana huko pia.
5. Baada ya kumkosa huko kote kamati ilienda idara ya uhamiaji makao makuu ili kujua kama Ben amesafiri nje ya nchi, lakini ilionekana kwamba Ben hajasafiri nje ya nchi kwa kipindi cha mwezi November wala December.
Taarifa ya Idara ya uhamiaji kuwa Ben hajasafiri nje ya nchi ilitoa tafsiri kuwa Ben bado yupo nchini. Lakini maswali yanabaki yupo wapi? Yupo katika hali gani? Je amekufa au yupo hai? Kwanini taarifa zake hazipo wazi?
6. Kufuatia sintofahamu hiyo kamati ilienda mamlaka ya mawasiliano nchini TCRA ili kupata taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben ambazo zingesaidia kufumbua kitendawili cha alipo Ben.
TCRA waliieleza kamati kuwa jukumu hilo ni la kampuni ya simu kupitia jeshi la Polisi, na hivyo Polisi wanapaswa kuandika barua kwenye kampuni husika ya simu kuomba taarifa za mawasiliano ya Ben. Polisi walichukua upya maelezo ya tukio hilo na kuahidi kuandika barua hiyo kwenye kampuni husika ya simu ili kupata mawasiliano yake.
Lakini hadi sasa kamati hiyo haijapata mawasiliano hayo kwa madai kuwa bado kampuni husika ya simu haijawasilisha taarifa hiyo kwa jeshi la Polisi.
7. Tarehe 08/12/2016 ziliripotiwa taarifa za kuokotwa kwa miili ya watu huko Bagamoyo eneo la mto Ruvu. Kwa kuwa familia na uongozi wa UTG zilikua katika taharuki ya kupotea kwa Ben kamati ililazimika kusafiri kwenda Bagamoyo kujiridhisha kama miili iliyookotwa inahusiana na Ben kwa namna moja au nyingine.
Kamati inayofuatilia suala hili ilipofika ilikuta miili yote imeshazikwa bila kuacha kielelezo chochote. Tarehe 09/12/2016 kamati ikiwa bado Bagamoyo ilishuhudia maiti nyingine moja ikielea katika mto Ruvu, eneo lilelile zilipopatikana maiti za awali. Polisi walifika na kuichukua maiti hiyo, na ilipoikaguliwa iliridhika kuwa sio ya Ndugu Ben Saanane.
*2. KUOKOTWA KWA MIILI YA WATU 7 KATIKA ENEO LA MTO RUVU, KATA YA MAKURUNGE, WILAYANI BAGAMOYO.
Ndugu waandishi wa habari,
Kama tulivyowaeleza hapo awali kuwa iliokotwa miili ya watu 6 siku ya jumatano tarehe 7/12/2016 katika kingo za mto Ruvu kijiji cha Mtoni, kata ya Makurunge na maiti nyingine moja ijumaa ya tarehe 09/12/2016 katika eneo hilohilo na kufanya jumla ya maiti zilizopatikana kuwa 7.
Taarifa ya kupatikana miili hiyo ni ya kuogofya na kushtua hasa kutokana na namna miili hiyo ilivyookotwa.
Miili 6 ya awali ilikua imewekwa ndani ya mifuko ya sandarusi na ndani iliwekewa mawe ili isielee, kisha mifuko hiyo kushonwa na kutupwa mtoni. Mwili mwingine mmoja uliopatikana tarehe 09 haukua ndani ya sandarusi lakini ulikua umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni na kwenye ubavu kama vile umejeruhiwa na kitu chenye ncha kali.
Mazingira ya kupatikana kwa maiti hizo na hali ilizokua nazo ni viashiria kuwa sio vifo vya kawaida.
Mazingira ya maiti hizo yanaashiria vitu viwili. Mosi huenda watu hao waliuawa kabla ya kutupwa mtoni au walijeruhiwa kabla ya kuwekwa kwenye mifuko hiyo wakiwa hai na kutupwa katika mto huo na kufia humo.
Sisi kama Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania tunasikitika sana kuona jambo hili la vifo vya watanzania wenzetu likipewa uzito mdogo na taasisi zenye wajibu wa kushughulikia jambo hili.
Ni ajabu kwamba hadi Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Pwani haijachukua hatua zinazoridhisha juu ya jambo kubwa kama hili. Taarifa tuliyoipata kutoka ofisi ya serikali ya kijiji cha Makurunge inaeleza kuwa hadi kufikia tarehe 10/12/2016 hakuna kiongozi yeyote wa serikali kuu aliyekua amefika eneo hilo. Si Waziri, Mkuu wa mkoa wa Pwani wala Mbunge wa eneo husika waliokua wamefika eneo hilo.
Ni jambo la kustaajabisha kwamba watu 7 wanaweza kupoteza uhai wao katika mazingira yenye utata na serikali isichukue hatua za kuridhisha wala Waziri kutoa tamko. Ikumbukwe ni serikali hiihii ambayo mawaziri wake watatu walitoa tamko kufuatia mwanafunzi mmoja kuadhibiwa huko mkoani Mbeya na waalimu wa mazoezi kwa madai kuwa ni ukatili, lakini hakuna Waziri yeyote aliyetoa tamko kuhusiana na suala la miili iliyookotwa Bagamoyo.
Ikiwa adhabu kwa mwanafunzi ilipewa uzito na kufanya mawaziri watatu kutoa tamko, lakini hakuna waziri hata mmoja aliyetoa tamko kwenye suala hili la Bagamoyo, sisi kama umoja wa kizazi cha kuhoji tunatilia shaka utendaji wa serikali.
Haiwezekani adhabu kwa mwanafunzi mmoja iwe na uzito mkubwa kuliko uhai wa watanzania 7. Serikali inayoona adhabu kwa mwanafunzi mmoja ni ukatili kuliko vifo vya watanzania 7 ni serikali isiyojali watu wake.
Serikali imekaa kimya kuhusu maiti 7 zilizookotwa Bagamoyo lakini ipo busy kufuatilia suala la kupotea kwa Faru mmoja aitwae John katika hifadhi ya Ngorongoro. Suala la Faru huyo limepewa uzito mkubwa kiasi cha baadhi ya mawaziri kuhangaika usiku na mchana kujua alipo Faru huyo, lakini suala la vifo vya watanzania wenzetu na miili yao kutupwa mto Ruvu halijapewa uzito wowote.
Haiwezekani katika taifa letu Faru mmoja awe na thamani kuliko maisha ya watanzania 7. Hatumaanishi kuwa suala la Faru lipuuzwe, hapana. Tunamaanisha suala la Faru lipewe uzito lakini suala la vifo vya watanzania wenzetu lipewe uzito zaidi. Tunathamini rasilimali za nchi lakini tunapaswa kuthamini zaidi maisha ya watanzania. Rasilimali zetu hazitufai kitu ikiwa maisha yetu hayathaminiwi.
Tunaamini Waziri wa mambo ya Ndani Mhe.Mwigulu Nchemba ni mtendaji mzuri na anayechukua hatua kwa wakati katika mambo yanayohusu wizara yake. Hata lilipotokea tulio la mauaji ya askari kule Chamazi (Mbande) Mhe.Mwigulu alifika eneo la tukio usiku huohuo. Lakini tumeshangazwa na ukimya wake kwenye suala hili la kuokotwa kwa miili ya watanzania wenzetu huko Bagamoyo.
Tumesikitishwa pia na kitendo cha Jeshi la Polisi kuamua kuizika miili hiyo bila kuacha vielelezo vyovyote huku jeshi hilo likiwa na taarifa ya baadhi ya watanzania kupotelewa na ndugu zao. Hii si sahihi hata kidogo.
Wapo watanzania wametoa ripoti za kupotelewa na ndugu zao katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, ikiwemo familia ya Ndugu Ben Saanane, sasa kwanini polisi waamue kuzika miili hiyo bila kusubiri uchunguzi?
Utetezi uliotolewa na Polisi kwamba miili hiyo ilikua imeharibika hauna mashiko kwani tunaamini vingeweza kupatikana vinasaba ambavyo vingewasilishwa ofisi ya mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Lakini Polisi kuamua kuizika miili hiyo bila hata kuacha vipande vya nguo za marehemu ni jambo linalotilia shaka weledi wa jeshi hili.
Pia eneo ilipokutwa miili hiyo halina doria wala ulinzi wowote nyakati za usiku. Utafiti ulioufanywa na kamati unaonesha kuwa eneo hilo limekuwa na historia ya matukio ya kutisha kwa muda mrefu lakini halina ulinzi wowote.
Pia kupatikana kwa miili ya watu 6 waliowekwa kwenye mifuko ya sandarusi iliyojazwa mawe ndani ni kielelezo kuwa maiti hizo hazikutupwa mbali na eneo hilo. Si rahisi maiti zisafirishwe kwa maji kwa eneo kutoka nje ya Bagamoyo wakati zina mawe ndani na bila mifuko iliyohifadhia haijaharibika.
Kama maiti hizo zilisafirishwa kwa magari kutoka maeneo ya mbali zikiwa kwenye mifuko na kwenda kutupwa eneo hilo inawezekanaje wakati njiani kuna askari polisi wanaokagua magari?
Na ikiwa watu hao walisafirishwa wakiwa hai kama mateka na kwenda kuuawa eneo la jirani na mto huo na kuwekwa kwenye mifuko ya sandarusi na kutupwa mtoni, je inawezekanaje watu 7 kusarishwa kama mateka bila Polisi kujua? Bado maswali ni mengi kuliko majibu.
Vilevile tunasikitishwa na kitendo cha Idara ya Afya wilaya ya Bagamoyo kushindwa kuchukua hatua. Baada ya maiti hizo kuonekana eneo hilo la mto bado watu waliendea kutumia maji ya mto huo katika matumizi mbalimbali.
Kamati ilifika eneo hilo na kushuhudia maiti zikiwa mtoni na pembezoni kidogo wananchi wakichota maji ya kunywa, ya kupikia na shughuli zingine. Maana yake ni kwamba kuna watu walikunywa, na kupikia maji yaliyotokana na maiti. Hii ni hatari sana kwa afya za wakazi wa kata ya Makurunge na maeneo jirani kwa sababu inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.
Pia tunasikitishwa na utaratibu uliotumika kuizika miili iliyookotwa, kwa sababu haikuzikwa kama binadamu, wala haikupewa heshima bali ilifukiwa katika shimo moja watu wawili. Tunaamini binadamu anastahili kusitiriwa na kupewa heshima hata anapokua maiti, kwa hiyo haikua busara kuzika maiti mbili kwenye shimo moja tena kwa kuwafukia tu kwenye mashimo kama mizoga.
MAPENDEKEZO:
Kutokana na matukio hayo mawili hapo juu (la kupotea kwa Ndugu Ben Saanane na kuokotwa kwa miili ya watu 7 huko Bagamoyo, UTG inatoa mapendekezo yafuatayo:
1. Vyombo husika kutoa taarifa ya mawasiliano ya Ndugu Ben Saanane kama yalivyoombwa na familia yake. Tunasikitika sana kwa uhirikiano hafifu kamati iliopata kutoka Jeshi la Polisi na kampuni husika ya simu ambayo Ben alikua akitumia mtandao wao.
Tangu taarifa hiyo imeombwa kumekua na uchelewashwaji bila sababu zozote za msingi licha ya kukamilisha taratibu zote za kisheria zinazotoa haki ya kupata mawasiliano hayo.
2. Vyombo vya habari vitoe uzito kwenye matukio yanayohusu uhai wa watanzania kuliko matukio mengine yoyote kwa sababu uhai wetu ni muhimu kuliko jambo jingine lolote. Tumesikitishwa kuona magazeti yote yaliandika habari ya Faru aliyepotea Ngorongoro lakini ni gazeti moja tu lililoandika habari za kupotea kwa ndugu Ben Saanane. Pia ni magazeti machache yaliyoandika habari za maiti zilizopatikana Bagamoyo.
Tunawataka waandishi wa habari wazingatie weledi katika kuandika. Moja ya mambo yanayoweza kuipa uzito habari ni suala la ukubwa wa habari yenyewe (magnitude). Ni ajabu kwamba habari ya kupotea kwa Faru mmoja imeonekana kubwa kuliko kupotea kwa mtanzania mwenzetu Ndg.Ben Saanane au kuokotwa kwa miili ya watanzania wenzetu huko Bagamoyo.
3. Tunakitaka chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ambayo ndiyo taasisi Ben Saanane aliyokua akiifanyia kazi, kuchukua hatua za kiridhisha dhidi ya suala hili. Zipo taarifa kwamba Chadema wanafuatilia jambo hili na watachukua hatua, lakini sisi kama UTG hatujaridhishwa na namna chama hicho kinavyochelewa kuchukua hatua. Ben amekua mtumishi wa Chadema wa muda mrefu, hivyo hatuoni kama ni sahihi kwa chama hicho kushindwa kutoa tamko lolote hadi leo, ikiwa ni siku 24 sasa tangu apotee.
4. Tunazitaka taasisi zote za haki za binadamu zijitokeze hadharani na kupiga kelele juu ya mambo haya mawili makubwa katika taifa. Zipige kelele Ben apatikane akiwa hai, na zipige kelele Serikali ichukue hatua dhidi ya maiti zilizookotwa Bagamoyo.
Ikiwa Watanzania wanaweza kupotea na wasijulikane walipo, na wengine kuokotwa wakiwa maiti na wasijulikane walipotoka ni dalili kwamba nchi hii sio salama. Ziko wapi taasisi kama Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu? Iko wapi Tume ya Haki za binadamu na Utawala bora? Wanasubiri nini kutoa tamko juu ya mambo haya yanayotishia usalama wa raia?
5. Jeshi la Polisi liimarishe doria katika eneo la mto Ruvu mahali palipokutwa maiti hizo, na maeneo mengine kando ya mto huo yenye changamoto za kiusalama. Pia Jeshi hilo lifanye uchunguzi na kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kuhusika na matukio hayo.
6. Tunaitaka serikali kwa kushirikisha taasisi zake kama wizara ya afya, ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, na jeshi la polisi iratibu zoezi la kufukua miili iliyozikwa ili kupata sampuli zitakazotumika kutambua ndugu wa marehemu watakapojitokeza.
7. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo zijitathmini kuona kama zinastahili kuendelea kuwepo madarakani. Ikiwa mkuu wa mkoa wa Pwani hajafika eneo la tukio siku 4 baada ya maiti hizo kupatikana ajitathmini kama bado anastahili kuendelea kuongoza mkoa huo.
Mamlaka yake ya uteuzi pia ifikirie upya juu ya nafasi yake. Wapo wakuu wa mikoa na wilaya wanaowajibika na kuchukua hatua katika mambo yanayohusu raia. Tumeshuhudia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akishughulikia matatizo mbalimbali ya wananchi hata katika ngazi ya mtaa, lakini mkuu wa mkoa wa Pwani ameshindwa hata kutoa tamko tu la kulaani kitendo kilichotokea mkoani kwake.
8. Jukumu la kwanza la Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Ikiwa Polisi mkoa wa Pwani umeshindwa kutimiza jukumu hili, basi Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani na Wilaya ya Bagamoyo wajitathmini kama bado wanastahili kuendelea kuwepo katika nafasi zao.
9. Pia kitendo cha Mbunge wa Bagamoyo Prof.Shukuru Kawambwa kushindwa kufika eneo la tukio hata kutoa pole kwa wakazi wa kijiji cha Mtoni na Kata ya Makurunge kinatosha kumfanya ajitathmini kama kweli yeye ni mwakilishi wa wananchi.
10. Pia idara ya afya wilaya ya Bagamoyo ijitathmini na iwajibike kwa kushindwa kuchukua hatua kulinda afya za wakazi wa maeneo ilipookotwa miili hiyo. Ikiwa watu walikunywa, kuoga na kupikia maji yaliyogusana na maiti za binadamu, na idara ya Afya haikuchukua hatua yoyote basi ina kila sababu ya kuwajibika.
Mwisho tuhitimishe kwa kunukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere aliyosema kuwa "Binadamu wote ni ndugu, na Afrika ni moja. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuulinda, kuutetea na kuuthamini utu wa binadamu mwingine". Kwa maneno hayo ya Nyerere tunataka serikali ichukue hatua ya kumtafuta na kumpata Ndugu Ben Saanane akiwa hai, na serikali ichukue hatua za kuridhisha dhidi ya miili ya watanzania wenzetu iliyookotwa huko Bagamoyo.
Asanteni,
Imetolewa na:
Malisa Godlisten,
M/kiti UTG
Noel Shao
Naibu Katibu UTG.

Maoni