WANAFUNZI WALIOLIPUKIWA BOMU KAGERA SASA HAWAONI

 

Siku ya na moja baada ya mlipuko wa bomu uliotokea Shule ya Msingi Kihinga mkoani Kagera, majeruhi wawili wamerejeshwa hospitali baada ya kupata tatizo la kuona.

Watoto hao wawili ni miongoni mwa majeruhi 43, akiwemo mwalimu, wa mlipuko wa bomu uliotokea Novemba 8 na kuua wanafunzi watano baada ya mmoja wao kuliokota na kwenda nalo shuleni akidhani kuwa ni chuma chakavu ambacho angekiuza.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Misheni ya Rulenge, Dk Mariagoreth Frederick alisema jana kuwa watoto hao waliruhusiwa kurejea nyumbani Novemba 10 na walirejeshwa Novemba 14 kutokana na kuathirika machoni.

Aliwataja watoto hao kuwa ni Irene Sherehe na Domina Wabandi (10).

Dk Mariagoreth alisema Domina anafanyiwa utaratibu na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ili apelekwe Hospitali ya Rufaa ya KCMC ili kuwekewa jicho la bandia.

Bomu hilo lililipuka wakati wanafunzi wa darasa la kwanza wakiingia darasani na liliokotwa na mwanafunzi ambaye alilihifadhi kwenye begi lake la madaftari kwa lengo la kwenda kuliuza kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu.

Mbali ya hao, Dk Mariagoreth alisema watoto wengine wawili jana walihamishiwa Hospitali ya Kagondo wilayani Muleba ambako kuna madaktari bingwa wa mifupa.

Pia, alisema leo watawaruhusu majeruhi watano kurejea nyumbani kutokana na afya zao kuimarika, hivyo watabaki watano.

Majeruhi waliohamishiwa Hospitali ya Kagondo ni Emanuel Hilali (13) ambaye anahitaji uchunguzi zaidi wa mguu wa kushoto na ambaye pia alipoteza jicho la kulia lililoondolewa kutokana na kuharibika.

Mwingine ni Simon Boniface (10), mwenye tatizo kwenye kidevu na anahitajiwa kuchunguzwa meno yake. Pia, ana maumivu mguu wa kulia.

Dk Mariagoreth alisema bado wanahitaji dawa na vifaa tiba.

Alisema gharama za matibabu zilizotumika kwa majeruhi 33 walioruhusiwa ni Sh1.827 milioni na kwa waliopo hadi Novemba 14 wamefikisha Sh4.061 milioni.

“Wazazi wa majeruhi hawajiwezi kiuchumi, hivyo uongozi wa wilaya ulishauri watafutwe madaktari bingwa watoe huduma hapa badala ya kuwasafirisha kwenda hospitali za rufaa ili kupunguza gharama,” alisema.

Alisema majeruhi wanne ambao kila mmoja amepoteza jicho moja, hivyo wanatibiwa majeraha na mipango inafanywa ili fedha zikipatikana pia wapatiwe miwani ili kuongeza uwezo wao wa kuona kwa jicho lililobaki.

Dk Mariagoreth alisema wanahitaji dawa za antibiotiki kwa ajili ya kukausha vidonda vya majeruhi.

Jukwaa la Maendeleo ya Wakazi wa Rulenge na Murusagamba wilayani Ngara zlmechangia Sh1.07 milioni kusaidia mahitaji mbalimbali kwa ajili ya majeruhi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele aliyefika hospitalini kuwajulia hali majeruhi mwishoni mwa wiki, aliwataka wazazi na walezi kuwa na imani na madaktari wanaoshughulikia afya za watoto wao.

Alisema Serikali ya wilaya inafanya kila jitihada kuhakikisha huduma muhimu zinatolewa kwa majeruhi na baada ya kupona kutafanyika utaratibu wa kuhakikisha wanaendelea na masomo.

Pia, aliwashukuru wananchi wanaojitokeza kutoa misaada kupitia ofisi yake na kwa uongozi wa hospitali kwa kuonyesha uzalendo na kuwajali wenye shida.

Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi

Maoni