Serikali Kenya yapiga marufuku maandamano miji mikuu

Serikali nchini Kenya imepiga marufuku maandamano katika maeneo ya katikati mwa miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.
Kaimu waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i amesema pia kwamba wanaopanga maandamano wanafaa kuwajibishwa kutokana na uharibifu wa mali unaotokea wakati wa maandamano.
Hatua ya Dkt Matiang'i imetokea huku muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) wake Raila Odinga ukiendelea na maandamano ya kushinikiza mageuzi katika Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Jumatano, visa vya uporaji wa mali viliripotiwa katikati mwa jiji la Nairobi.
Mmoja wa viongozi wa Nasa James Orengo, ambaye alikuwa naibu ajenti mkuu wa Bw Odinga wakati wa uchaguzi wa mwezi Agosti ambao ulifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu, alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kuandamana kila siku.
Muungano wa Nasa awali ulikuwa ukifanya maandamano kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mageuzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.
Uchaguzi ambao umepangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba umeingiwa na utata baada ya mgombea wa Nasa Raila Odinga kutangaza kujiondoa rasmi Jumanne.
Mapema Jumatano, Mahakama Kuu pia iliagiza mgombea wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot ajumuishwe kwenye uchaguzi huo.

Maoni