JINSI TUNDU LISSU ALIVYOSHEREHEKEA MIAKA 20 YA NDOA AKIWA KITANDANI NAIROBI LEO KWA SHAMBULIO KUBWA LA KUPIGWA RISASI DODOMA TANZANIA.
Utafanya kitu gani ukitimiza miaka 20 ya ndoa? Au ulifanya nini ulipotimiza miaka hiyo ya ndoa?
Kila mmoja huwa na utaratibu wake ambao
huambatana na uwezo wa kiuchumi ili kuiweka kumbukumbu hiyo ya ndoa
vizuri na ndio maana kuna ambao hufanya sherehe kubwa na wengine
hukumbuka kwa ‘maneno tu’.
Iwe ni kumbukumbu ya miaka mitano, 10 au
15, huwa ni muhimu kutafakari muunganiko wa watu wawili ambao wameishi
pamoja wakipita milima, mabonde na kuvuka vihunzi vingi.
Iwe ni kwa sherehe au ‘maneno makavu’
tu, siku hiyo huwa ni muhimu kuitafakari na ikiwezekana wawili hao, huwa
wanatathmini walikotoka na wanakokwenda.
Lakini, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mkewe Alicia, wana stori tofauti kuhusu kumbukumbu ya ndoa yao.
Leo Jumatano, Novemba 29, Lissu na
Alicia wanatimiza miaka 20 ya ndoa yao, lakini wanatafakari safari hiyo
ndefu ya muunganiko wao wakiwa mazingira tofauti;Hospitali ya Nairobi.
Wanaweza kuitumia siku ya leo kulishana
keki, lakini Lissu anatimiza siku 84 akiwa Hospitali ya Nairobi huku
mkewe, Alicia akiwa kando ya kitanda kumhudumia kwa siku zote hizo.
Lissu aliyepigwa risasi zaidi ya 30
akiwa ndani ya gari lake nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba
7, mwaka huu anazungumzia kumbukumbu ya miaka 20 akiwa amejilaza
kitandani hospitalini hapo katika mahojiano na Mwananchi.
“Mke wangu nikuzungumziaje? Lissu anamuuliza Alicia ambaye anamjibu, “kazi kwako.”
“Mke wangu mpenzi anaishi kiapo chake
tulipooana Novemba 29, 1997, tunatimiza miaka 20 …tulipooana nilimsikia
anasema ‘kwa shida na raha, nitampenda, nitafanya nini na nini’, kwa
hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” anasema Lissu akiwa
mwenye tabasamu.
“Katika miaka hii 20, tumepitia
majaribu mengi sana, lakini hili (kupigwa risasi) ndilo kubwa kuliko
yote na nafikiri kama ni mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu
kabisa kwa sababu amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia
anavyozungumza ana msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa,” anasema
mwanasheria huyo.
“Ni mke wa kweli, aliyekubali kuchukua
majukumu ya kuwa mke, najisikia faraja na furaha ya kipekee kwa sababu
ya kuwa naye na ninamwomba tuendelee kuwa hivyo kwa miaka 20 mingine
inayokuja,” anasema Lissu huku pembeni yake mkewe akitabasamu.
Anatumia muda huo kumpa ujumbe mke wake
kuwa, “najisikia mwanamme mwenye bahati sana kuwa naye, ni mwanamke wa
kipekee sana kuwa naye, tumetoka mbali sana na hii miaka 20 imekuwa
mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa naye.”
Alicia hakuacha mazungumzo hayo yapite hivi hivi tu, alikuwa na mtazamo wake kuhusu safari hiyo ya miaka 20.
“Miaka 20 ni mingi, lakini nikifikiria
ni kama juzi tu, halafu nilikuwa sitaki kumkumbusha nilitaka kumfanyia
‘surprise,’” anasema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na kutabasamu.
Alicia, ambaye kitaaluma ni wakili
anasema, “lazima niwe mkweli kuna miaka mingine ilikuwa busy anasahau
hata siku…Tundu ni mume wangu, kikubwa naweza kusema ni rafiki yangu wa
karibu sana wa miaka mingi sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na smati,
tumekuwa tukiishi hivyo.”
“Ujumbe wangu, Tundu siku zote aendelee
kuwa Tundu tu, Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe ni Tundu
niliyemjua siku zote,” anasema.
Tundu Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ametimiza siku 84 tangu alipopigwa
risasi mjini Dodoma na kusafirishwa kwa ndege kwenda kutibiwa katika
Hospitali ya Nairobi.
Maoni
Chapisha Maoni