SERIKALI YAJA NA MAELEZO TOFAUTI JUU YA UPANDISHWAJI WA MISHAHARA NA VYEO NA KUWAACHA MIDOMO WAZI WAFANYAKAZI.
HATIMAYE serikali imetoa vigezo vinavyotakiwa kutumika kama vipaumbele wakati wa kuwapandisha watumishi wa umma mshahara.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro ndiye aliyetangaza vigezo hivyo
vinavyopaswa kutumiwa na waajiri katika utumishi wa umma kuwapandisha
watumishi mishahara.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ndumbaro,
suala la upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma litazingatia zaidi
utendaji kazi wa mtumishi husika na si suala la sifa ya Muundo wa
Utumishi (Scheme of Service) pekee kwa maana ya muda wa kutumikia miaka
mitatu mitatu kama wengi wanavyodhani.
Aliyasema hayo kwa wakati tofauti katika
Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Namtumbo na Manispaa ya Songea katika
ziara yake ya kikazi ya siku tano ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma.
Katibu Mkuu Ndumbaro alisisitiza kuwa
mtumishi wa umma anayewajibika vizuri katika utendaji kazi wake wa kila
siku ndiye atakayepandishwa cheo na si vinginevyo.
Alilazimika kutoka ufafanuzi huo,
kufuatia baadhi ya watumishi katika halmashauri hizo kulalamika
kutopandishwa madaraja (vyeo) kwa wakati kwa muda mrefu sasa wakati
wenzao walioanza nao kazi wameshapandishwa vyeo, hivyo kusababisha uwepo
wa tofauti kubwa ya mishahara baina yao.
“Haiwezekani Serikali ikapandisha
mishahara kwa watumishi wasiowajibika, walevi na wasio na nidhamu na
uadilifu katika utendaji wao wa kazi, atakayewajibika katika utendaji
wake ndiye atakayepandishwa ngazi ya mshahara,” alisisitiza.
Katibu Mkuu huyo aliainisha kuwa,
malalamiko mengi ni ya walimu ambao wamekuwa wakidhani kuwa kila baada
ya miaka mitatu lazima wote wapandishwe vyeo (madaraja) hata kama
hawajawajibika ipasavyo, suala ambalo si sahihi.
“Haiwezekani Mwalimu anayefundisha
vizuri darasani na wanafunzi wake wanafaulu vizuri masomo yake
akapandishwa daraja sawasawa na yule ambaye ufundishaji wake hauridhishi
na ni mlevi wa kupindukia hali inayochangia wanafunzi wengi kutofaulu
somo lake.”
Aidha alisema hivi karibuni, ofisi yake
inatarajia kukutana na Tume ya Utumishi wa Walimu na kuzungumza na
Walimu ili kutoa elimu na ufafanuzi yakinifu wa vigezo vya msingi
vinavyozingatiwa katika suala la upandishaji vyeo kwa watumishi wa umma
nchini kwa lengo la kuepukana na malalamiko yasiyo ya lazima.
Chanzo- Habarileo
Maoni
Chapisha Maoni