Serikali yazuia uzinduzi wa ripoti ya HRW

 

Serikali ya Tanzania imezuia uzinduzi wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa wafanyakazi wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi za ndani katika mataifa ya Oman na Falme za Kiarabu.

Shirika la Human Wrights Watch limedai kuwa katika matokeo yake ya utafiti uliofanyika kwa wafanyakazi wa nyumbani kutoka nchini Tanzania walikuwa wakibakwa, kuteswa na kulipwa mishahara duni na waajiri wao katika mataifa ya Uarabuni.

Katika Ripoti iliyotolewa yenye kurasa 100 inayodai kuteswa kwa wafanyikazi wa nyumbani kutoka Tanzania nchini Oman na muungano wa mataifa ya Emirate UAE ilitarajiwa kutolewa kwa waandishi wa habari mbele ya waathiriwa lakini hilo halikufanyika.

Aidha, katika hali isiyokuwa ya kawaida ,Afisa mmoja kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia COSTEC, William Kindekete alizuia kufanyika kwa mkutano huo na waandishi wa habari jijini Dar es salaam akisema kuwa wanaharakati wa shirika hilo la haki za kibinaadamu hawakufuata taratibu za sheria katika kufanya utafiti wao.

 Matokeo ya utafiti huo wa HRW umeonyesha kuwa takriban wanawake 50 walihojiwa wakati wa utafiti huo ambao wanadai kuwa walilazimishwa kufanya kazi kwa kati ya saa 15 na 21 kwa siku huku wakipokonywa pasipoti zao na waajiri wao punde tu walipowasili katika mataifa hayo.

Hata hivyo, ripoti hiyo ya HRW pia imesema kuwa balozi za Tanzania katika eneo la Ghuba hazikutoa usaidizi wowote kwa waathiriwa wakati walipotaka usaidizi ili kuweza kuepukana na matatizo

Maoni