Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu amesimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio na pia kueleza
ujumbe aliompa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipomtembelea
hospitalini jijini Nairobi juzi.
Mbunge huyo, ambaye alishambuliwa kwa
risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma
Septemba 7, pia amesema amepitia majaribu mengi, lakini “hili ndilo
kubwa”.
Amesema hali yake inaendelea vizuri na
madaktari wanamuelezea kuwa ni “muujiza unaoishi” baada ya kufanikiwa
kuunganisha vipande vya mwili ulioharibiwa kwa risasi.
Lissu alisema hayo alipofanya mahojiano
na Mwananchi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Tanzania
tangu ashambuliwe.
Lissu amelazwa Hospitali ya Nairobi
jijini hapa tangu Septemba 7 na huenda akahamishiwa nje ya bara la
Afrika kwa matibabu zaidi, ambayo yatahusu mazoezi, kabla ya kurejea
nchini.
Akizungumza na Mwananchi hospitalini
hapo, Lissu alisema sasa anaamini kuwa Rais John Magufuli anajua kuna
mgonjwa Nairobi na hivyo kufungua milango kwa wengine waliokuwa na hofu.
“Mimi namuamini na naendelea kuamini
kwamba kwa sababu sasa Makamu wa Rais amekuja kwa niaba ya Rais,
ametambua tuna mgonjwa yupo Nairobi. Milango itafunguka kwa wale wengine
wote waliokuwa na hofu ya kuja,” alisema Lissu.
“Sasa Rais mwenyewe kamtuma makamu wake kuja kunipa pole, kwa hiyo hao wengine wa taasisi zote hawana hofu ya kuja kuniona.”
Akizungumzia mazungumzo yake na Suluhu, Lissu alisema yalikuwa mazuri.
“Mama Samia ni kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Tanzania pamoja na mihimili yake kuja kunitembelea,” alisema Lissu.
“Spika wa Bunge hajaja, katibu wake na
uongozi mzima wa Bunge haujaja. Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi hawajaja
pamoja na kwamba mimi ni Rais wa TLS.
“Na kwa kawaida mila na desturi za
mahakama zetu, bila mawakili hakuna mahakama na kama Rais wa TLS
nimekuwa nikialikwa na kuhudhuria vikao mbalimbali vya kiutendaji,
lakini tangu nimeshambuliwa Jaji Mkuu au uongozi mzima wa Mahakama hata
kutoa salamu za pole, hakuna.
“Rais Magufuli alikuwa hajawahi kusema
lolote kuhusu kushambuliwa kwangu kama nakumbuka, lakini leo (juzi)
amekuja Makamu wa Rais na amenieleza na napenda kuamini ni kweli
ametumwa na Rais kama sehemu yake ya shughuli zilizomleta Kenya apitie
kunisalimia na kunipa pole.”
Alisema Makamu wa Rais, ambaye waliwahi
kufanya naye kazi wakati akiwa waziri anayehusika na Muungano na Lissu
akiwa waziri kivuli wa eneo hilo, alimuuliza kama ana jambo lolote la
kumweleza Rais, naye akamweleza kuhusu gharama za matibabu.
“Mimi bado ni mbunge, ujumbe ambao
nataka aupeleke ni Bunge liko wapi? Bunge ambalo lina wajibu wa kisheria
wa kunihudumia nikiwa naugua?” aliuliza Lissu akirejea mazungumzo hayo
na Suluhu juzi jioni.
“Nilimpa ujumbe huo na napenda kuamini
ataufikisha na ujio wake peke yake unatakiwa kufungua milango kwa wale
waliokuwa wanafikiri wamefungiwa.”
Alisema suala la Bunge kuwa mbali naye ni mfano mwingine unaotia shaka kuhusu kushambuliwa kwake.
“Mimi ni mbunge na ni Mnadhimu Mkuu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ninatambuliwa na Sheria za Tanzania,
Sheria inayohusika ni ya uedeshaji wa Bunge. Sheria inaeleza kwamba
mbunge anapoumwa atapata matibabu pamoja na gharama nyingine kutoka
bungeni,” alisema.
Lissu alisema kila mbunge anayeumwa
analipiwa gharama zote na Bunge na vile vile kama itabidi, alazwe nje ya
Dodoma iwe Dar es Salaam, Afrika Kusini, India Marekani au Kenya.
“Analipwa posho na Bunge na mtu
anayemuuguza analipwa posho vile vile, nusu ya posho ya mbunge ili
kumudu gharama za maisha,” alisema.
“(Lakini) Tangu nimeumizwa, Spika
anajua, alitangaza bungeni mbunge mwenzetu anaumwa. Tangu wakati huo
mpaka leo Spika hajaja, Katibu wa Bunge, Tume ya Bunge haijaja,” alisema
Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.
Alisema kuna wabunge wawili CCM, Mary
Chatanda (Korogwe Mjini) na Fakharia Shomar Khamis (viti maalum na
mmoja wa watumishi wa Bunge walifika siku ya Jumapili, siku ambayo si ya
kazi.
“Walikuja kunipa pole, walikaa hapa
wakanipa nipa pole, halafu wakaniaga. Nikawauliza mmetumwa chochote,
wakasema hapana,” alisema.
“Nikamuuliza ofisa wa Bunge, ‘kuna ujumbe umetumwa uniletee, akasema hapana. Kwa hiyo hao wawili walikuja kibinafsi tu.
“Tume ya Huduma za Bunge
inayoshughulikia mambo haya, haijaja mpaka leo. Kwa hiyo ukiachilia
mbali matangazo ya Spika, Bunge halijaja kabisa, halijanishughulikia kwa
lolote.
“Hakuna anayeomba fadhila, nataka haki,
nitendewe haki, anayetendewa mbunge yoyote anayeumwa. Hakuna anayelilia
fadhila hapa, hakuna anyeomba ufadhili. Nataka Bunge litimize wajibu
wake wa kisheria. Hili nitalipigania, kama siwezi kudai haki yangu ya
kisheria ambayo iko wazi, kama ya kwangu naona inakanyangwa kwa makusudi
tu, nitapigania ya nani?”
Lissu alisema Bunge halina sababu za maana za kutomgharimia, bali ni kupiga chenga tu.
“Wameandikiwa barua na ndugu yangu mara
hawajaiona, kwa hiyo lazima nipiganie haki yangu ili nipiganie haki za
wengine,” alisema.
Niliona watu wawili wenye silaha
Katika mahojiano hayo na Mwananchi
yaliyochukua takriban dakika 60, Lissu pia alielezea jinsi shambulio
dhidi yake lilivyofanyika Septemba 7, lakini tofauti na kauli ya ndugu
zake kuwa anawajua watu hao, alisema hawafahamu watu hao na kusisitiza
suala la wachunguzi kutoka nje.
“Nilitoka bungeni muda wa saa saba hivi,” alisema.
“Kabla sijatoka nilichangia mjadala wa
mkataba kati ya Malawi na Tanzania kuhusu Mto Songwe. Baada ya kumaliza
kuzungumza nikakaa kidogo kisha nikatoka na kwenda nyumbani kwa chakula
cha mchana.
Alisema alivyofika nyumbani, wakatokea
watu eneo la kuegesha magari katika nyumba hizo za Serikali, ambako
anaishi jengo moja na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mbunge wa
Ulanga Magharibi (CCM), Dk. Haji Mponda na mmoja wa makatibu wakuu wa
wizara.
“Kwa hiyo nakaa katika nyumba za
Serikali. Watu wameingia katika nyumba za Serikali zinazolindwa saa 24,
block inayotazamana na nyumba yangu, anakaa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
na huwa kuna polisi nje saa 24,” alisema.
“Lakini watu wameingia wenye silaha,
wakaja kunishambulia. Sikuwatambua kwa sababu nilishambuliwa nikiwa
katika gari sikutoka nje. Dereva wangu aliniambia kuna watu wako nyuma
wananifuata nisifungue mlango.”
Alisema alijaribu kuwaangalia kwa
kutumia kioo cha pembeni ya gari na kuwaona watu wawili wakitoka na
bunduki. Yaliyofuata nimekuja kujikuta nipo hapa nilipo leo wiki moja
baadaye.
“Kwa hiyo, siwezi kusema ninawafahamu
walionishambulia. Sikutambua hata mmoja wao ila najua nilishambuliwa na
watu wawili katika gari iliyokuwa na vioo vyeusi.”
Lissu alisema wiki tatu kabla ya
shambulio hilo alilalamika hadharani kwamba anafuatiliwa kila
anapokwenda na siku moja aliwasimamisha watu hao katika Kanisa Katoliki
la Mtakatifu Petro na kuwauliza sababu za kufanya hivyo.
“Niliwauliza kwa nini wananifuata na kama kuna mtu kawatuma, mwambieni mimi si mhalifu. Lakini sikupewa ulinzi wowote,” alisema.
Wachunguzi kutoka nje
Kama ilivyo kwa familia yake na Chadema, Lissu anataka uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na taasisi ya nje.
“Serikali inakosea sana,” alisema.
“Hili ni tukio la mbunge kushambuliwa
akiwa maeneo ya Bunge. Kisheria hayo maeneo yanayoitwa ya Bunge ni
pamoja na makazi ya wabunge wanapokuwa bungeni.”
Alisema huwezi kuwa bungeni kama huna sehemu ya kulala, kwa hiyo makazi yangu ni sehemu ya Bunge.
“Kitendo cha mbunge kushambuliwa wakati
vikao vinaendelea-- na mbunge mwenyewe ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni na anajulikana kwa kuikosoa Serikali mara nyingi kwa
muda mrefu, inatia shaka,” alisema.
“Kitendo hicho peke yake kingetosha
kutilia shaka uchunguzi wowote utakaofanywa na wale ambao mbunge huyo
amekuwa akiwasema mara kwa mara. Kitendo hicho kingetosheleza kualika
watu kutoka nje kuja kufanya uchunguzi.
“Wanakataa kwa sababu zao, tunaelekea
miezi mitatu, polisi hawajasema wanamshuku nani. Hakuna mtuhumiwa hata
mmoja halafu kuna jitihada kubwa imefanywa na Jeshi la Polisi kuzuia
raia kumsaidia huyu mbunge.”
Alisema polisi imewazuia watu wasisali,
wasimwombee Mungu apone, watu wasimchangie damu, kusiwe na dalili zozote
za wazi za kumuunga mkono na huyu ambaye ameshambuliwa na watu
wanasemekana hawajulikani.
“Kumekuwa na jitihada kubwa sana kuzuia
watu wasimsaidie huyu kuliko kufanya upelelezi, hiyo inatoa picha kwamba
bila uchunguzi huru ukweli hautajulikana, utafichwa na pengine ndivyo
wanavyotaka,” alisema.
Akizungumza huku akisisitiza kwa mikono
yake, Lissu alisema katika mlango wa Waziri Kalemani, kuangalia block ya
Naibu Spika Dk Tulia, kuna camera za CCTV zinazofanya kazi Saa 24 hivyo
kwa mtu yeyote ambaye yupo eneo hilo anaonekana, lakini akasema kuna
vitu vinaashiria kuwa kunahitajika jicho la pili kuangalia hili.
Alipoulizwa nafasi ya Rais Magufuli
katika suala hilo la uchunguzi, Lissu alisema: “Rais anaweza akitaka
kuelekeza. Polisi ndio wenye mamlaka ya kiuchunguzi, waalike wataalamu
kutoka nje.
“Haitakuwa mara ya kwanza, hatutakuwa wa
kwanza kufanya hivyo na haitakuwa aibu ila ni namna nzuri zaidi ili
kuondoa wingu lililotanda juu ya kushambuliwa kwangu, ukweli utajulikana
na hiki kimya si kizuri.”
Lissu pia alizungumzia hali yake kiafya na matarajio yake.
“Nafikiri kiafya Lissu anaendelea vizuri
na matibabu, hajapona bado lakini anaendelea vizuri, madaktari wanasema
hali yangu inakuwa inatengamaa kila siku,” alisema.
“Huko tulikotoka ni kurefu zaidi kuliko
tunakokwenda, vidonda vyote vya risasi vimepona, sina bandeji mwilini,
sina bandeji kabisa. Maana yake vile vidonda vyote vilivyotokana na
kupigwa risasi vimepoma.”
Hata hivyo, Lissu, ambaye chama na
familia yake imesema ataenda kumalizia matibabu nje ya bara la Afrika,
alisema bado hajajua ataruhusiwa lini, ingawa anajiona yuko katika hali
nzuri.
“Madaktari hawajanipa muda, na nafikiri
hawajanipa muda kwa sababu nzuri tu, majeraha niliyokuwa nayo
nilipoletwa hapa, yalikuwa makubwa sana, madaktari wenyewe wamekuwa
wakiniambia mimi ni muujiza unaoishi,” alisema.
“Kwa hali niliyoletwa hapa ni muujiza
unaoishi. Kazi kubwa walioifanya ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wanaokoa
maisha na wameokoa maisha. Kazi ambayo inafuata ni kuniwezesha kurudi
sasa katika hali yangu ya kawakida, kuweza kujitegema kimwili.”
Alisema madaktari wamemuwekea vyuma, wameunganisha mifupa.
Alisema mikono ilikuwa haifanyi kazi,
lakini sasa anaweza kuichezesha na kula na kwamba tiba hiyo inachukua
muda lakini tuko katika hatua ambayo si ya kuokoa maisha, bali ya
kurudisha mwili katika hali ya kawaida.
“Kimawazo nafikiri sijabadilika sana,
Lissu wa kabla ya Septemba 7 na Lissu wa leo kimsimamo wa kisiasa
hajabadilika kabisa. Lazima tupiganie demokrasia, hiyo ndiyo salama
yetu,” alisema.
“Tuwe na utawala wa kidemokrasia
unaojali haki za binadamu, tuwe utawala wa sheria, tuwe na mfumo wa
uongozi unaojali maisha ya wananchi, unaowajibika kwa wananchi au kwa
wawakilishi wake na huu ni msimamo wangu unajulikana na bado uko vile
vile.
Aadhimisha miaka 20 ya ndao wodini
Wakati akiendelea kutibiwa hospitalini
hapo, jana Lissu na mkewe, Alicia walitimiza miaka 20 tangu walipofunga
pingu za maisha Novemba 29, 1997 na kama kawaida walikuwa pamoja wodini.
“Mke wangu nikuzungumzieje?” alimuuliza.
“Kazi kwako,” Alicia alijibu.
“Mke wangu mpenzi anaishi kiapo chake
tulipooana na kesho (jana) tunatimiza miaka 20. Tulipooana nilimsikia
anasema ‘katika shida na raha’ nitampenda, nitafanya nini na nini’. Kwa
hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” alisema Lissu huku
Alicia akitabasamu.
“Katika miaka hii 20, tumepitia majaribu
mengi sana, lakini hili ndilo kubwa kuliko yote na nafikiri kama ni
mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu kabisa kwa sababu
amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia anavyozungumza ana
msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa.”
Lissu alisema Alicia “ni mke wa kweli,
aliyekubali kuchukua majukumu ya kuwa mke”, na kwamba anajisikia faraja
na furaha ya kipekee kuwa naye na angepende wawe pamoja miaka 20
mingine.
“Najisikia mwanamme mwenye bahati sana
kuwa naye. Ni mwanamke wa kipee sana kuwa naye. Tumetoka mbali sana na
hii miaka 20 imekuwa mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa
naye,” alisema.
Alicia pia alikuwa na lake moyoni.
“Miaka 20 ni mingi, lakini nikifikiria
kama ni juzi tu. Halafu nilikuwa sitaki kumkummbusha nilitaka kumfanyia
‘surprise (kumstua),” alisema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na
kutabasamu
“Lazima niwe mkweli. Kuna miaka mingine
alikuwa busy (na kazi nyingi), anasahau hata siku. Tundu ni mme wangu,
kikubwa naweza kusema ni rafiki yangu wa karibu sana wa miaka mingi
sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na smart. Tumekuwa tukiishi hivyo.”
“Ujumbe wangu, Tundu siku zote aendelee
kuwa Tundu tu. Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe ni Tundu
niliyemjua siku zote.”
Je, utagombea Urais 2020
Mbunge huyo wa Singida Mashariki hakutaka kuzungumzia uchaguzi wa mwaka 2020 na hata alipoulizwa kuhusu kugombea urais alistuka.
“Nafikiri huu ni mjadala unaohitaji kusubiri wakati mwafaka,” alisema.
“Si mjadala unaoweza kufanyika katika
kitanda cha Hospitali ya Nairobi, Kenya. ni mjadala unaohitaji tukae,
tushauriane. Kwa sababu ni chama lazima tukae tushauriane. Nafikiri hiki
kitanda changu si mjadala wa kuanzisha, kama watu wananitajataja huko
waendelee tu lakini mimi mjadala huu unisubiri nje ya hospitali.”Lakini
Lissu alisema kwa sasa atakuwa wa tofauti kwa kuwa amepitishwa tanuru la
moto na amepata uzoefu wa kutosha baada ya kujifunza mengi kutokana na
tukio la Septemba 7.
“Nikitoka hapa kama Mungu amenipa pumzi
ya kuendelea kuishi, haya mafunzo yatakuwa sehemu ya Lissu huyo baada ya
Septemba 7. Nimejifunza kuwa Watanzania ni watu wa upendo sana. Pamoja
na propaganda zote, uongo wote na ubaya wa watu, lakini Watanzania ni
watu wa upendo sana,” alisema Lissu
“Wanafahamu nani anawapigania. Kuna
rafiki yangu wa Dodoma ameniambia baada ya kupigwa risasi kuwa mji mzima
ulihamia hospitali. Ingawa siku zote CCM wanashinda pale, siku hiyo
walihamia pale (hospitali). Watanzania kila mahali walienda makanisani,
misikitini, nafikiria huo upendo nitaulipaje.
“Nafikiria ni upendo ni kwa sababu ya
kazi niliyoifanya bungeni na nje ya Bunge na hiyo kazi kama imewafanya
wawe na upendo namna hiyo, basi nitaizidisha na nitawafanyia kazi iliyo
bora zaidi.”
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni